Waziri wa Sheria wa Misri atimuliwa kwa kumvunjia heshima Mtume (saw)
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i2998-waziri_wa_sheria_wa_misri_atimuliwa_kwa_kumvunjia_heshima_mtume_(saw)
Waziri wa Sheria wa Misri, Ahmed al-Zand ametimuliwa kazi siku mbili baada ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) katika mahojiano ya televisheni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 13, 2016 22:34 UTC
  • Waziri wa Sheria wa Misri atimuliwa kwa kumvunjia heshima Mtume (saw)

Waziri wa Sheria wa Misri, Ahmed al-Zand ametimuliwa kazi siku mbili baada ya kumvunjia heshima Mtume Muhammad (saw) katika mahojiano ya televisheni.

Waziri Ahmed al-Zand ambaye Ijumaa iliyopita alizusha mjadala na makelele mengi nchini Misri baada ya kutoa matamshi yasiyofaa kuhusu Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) jana Jumapili alitakiwa na Waziri Mkuu wa Misri ajiuzulu wadhifa huo. Taarifa fupi iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu wa Misri imesema: "Waziri Mkuu, Sharif Ismail amemfuta kazi Waziri wa Sheria, Ahmed al-Zand".

hatua hiyo imechukuliwa baada ya kutoa matamshi yaliyomvunjia heshima Mtume Muhammad pale aliposema katika mahojiano na televisheni kwamba atamtia jela yeyote atakayevunja sheria hata akiwa Mtume (saw).

Uamuzi wa kutimuliwa kazi waziri huyo umechukuliwa baada ya kufanyika kikao cha dharura cha baraza la mawaiziri la Misri kilichojadili kadhia hiyo.

Baada ya matamshi hayo taasisi ya al Azhar nchini Misri ilitoa taarifa kuwa mtu yeyote anayezungumza na vyombo vya habari anapaswa kuwa macho na asimvunjie heshima Mtume (saw).

Hii si mara ya kwanza kwa Waziri wa Sheria kutoa matamshi kama haya yasiyofaa. Mwezi Januari mwaka huu Ahmed al-Zand alizindua mauaji ya halaiki dhidi ya wafuasi wa chama kilichopigwa marufuku nchini Misri cha Ikhwanul Muslimin pale aliposema kuwa "hataridhika bila ya kuua wanachama elfu kumi wa chama hicho mkabala wa mauaji ya kila mwanajeshi mmoja wa Misri au polisi yeyote atakayepoteza maisha katika ghasia na machafuko ya kitaani".