Viongozi wa dini: Wazanzibar waachwe wajiamulie wenyewe
Viongozi wa kidini wa Tanzania Bara na Visiwani wamekutana huko Zanzibar na kusisitiza juu ya hali ya amani visiwani humo. Aidha viongozi hao wametaka kupewa uhuru wa kuchagua wakazi wa visiwa hivyo katika uchaguzi wa marudio ujao ambapo wamesema kuwa ni jambo lisilo na mantiki kuwalazimisha wale wasiotaka kupiga kura kushiriki zoezi hilo.
Aidha viongozi hao kutoka dini za Kikristo, Kiislamu na Jumuiya ya Hindu wametaka kuhakikishwa usalama kwa wananchi watakaoshiriki kupiga kura katika uchaguzi huo na bila kubughudhiwa wale wasiopendelea kufanya hivyo. Katika sehemu nyingine viongozi hao wa kidini wamevitaka vyama vya siasa kuacha kutoa kauli za uchochezi ili kudumisha amani na usalama visiwani Zanzibar kwani kila mmoja ana wajibu wa kuhimiza suala hilo. Kikao cha viongozi hao kimefanyika kwa usimamizi wa taasisi ya Ujenzi wa Amani Tanzania (IRCPT). Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari hapo jana, imewanukuu viongozi hao wa kidini wakisema kuwa, wana wasi wasi kwamba kuna mgawanyiko miongoni mwa jamii unaosababishwa na tofauti mbalimbali zikiwemo za kisiasa huko Zanzibar suala ambalo ni hatari kwa usalama na amani ya visiwa hivyo. Aidha waliwapongeza Wazanzibari kwa kuwa wavumilivu na kulinda amani katika kipindi cha kuanzia uchaguzi uliopita wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana hadi sasa.