Sisitizo la Ufaransa na Ivory Coast la kuimarisha uhusiano baina yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30368-sisitizo_la_ufaransa_na_ivory_coast_la_kuimarisha_uhusiano_baina_yao
Marais Alassane Ouattara wa Ivory Coast na Emmanuel Macron wa Ufaransa wamesisitiza katika mazungumzo yao ya kwanza tangu Rais huyo mpya wa Ufaransa aliposhika hatamu za uongozi juu ya umuhimu wa kuimarisishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 12, 2017 10:53 UTC
  • Sisitizo la Ufaransa na Ivory Coast la kuimarisha uhusiano baina yao

Marais Alassane Ouattara wa Ivory Coast na Emmanuel Macron wa Ufaransa wamesisitiza katika mazungumzo yao ya kwanza tangu Rais huyo mpya wa Ufaransa aliposhika hatamu za uongozi juu ya umuhimu wa kuimarisishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ameashiria katika mazungumzo hayo mazingira ya kiuchumi ya Ivory Coast na kusisitiza juu ya azma ya nchi yake kuwa pamoja na nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika katika kusasisha na kuboresha uchumi wa nchi hiyo. Kuongezwa ushirikiano wa kijeshi, kupatiana taarifa na mafunzo sambamba na suala la vita vya pamoja dhidi ya ugaidi ni ajenda zingine zilizojadiliwa katika mazungumzo kati ya Marais hao.

Ivory Coast ni miongoni mwa nchi muhimu kwa Ufaransa barani Afrika. Hata kama wakati mwinginei uhusiano baina ya nchi mbili hizo umekuwa ukikabaliwa na mzozo wa kisiasa, lakini kuhifadhi uhusiano wake na Ivory Coast daima ni jambo ambalo limekuwa likipewa umuhimu na Paris. Suala la uchumi katika mazingira ya hivi sasa ni jambo linalozingatiwa zaidi na nchi mbili hizo.

Rais Alassane Ouattara wa Ivory Coast

Katika upande mmoja Ufaransa inakabiliwa na tatizo kubwa la kiuchumi likiwemo suala la ukosefu wa ajira, kiasi kwamba, moja ya ahadi za Rais Macron katika kampeni zake za uchaguzi ilikuwa ni kuyapatia ufumbuzi matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo hususan kupunguza kiwango cha ukosefu wa ajira. Katika upande wa pili, Ivory Coast nayo licha ya kuwa katika miaka ya hivi karibuni imepitia kipindi cha ukuaji mzuri wa uchumi, lakini kwa miezi kadhaa sasa inakabiliwa na matatizo ya kiuchumi hasa baada ya kuporomoka kwa bei ya kakao katika soko la kimataifa, bidhaa ambayo huiingizia nchi hiyo pato kubwa la kigeni.

Hali ya kiuchumi ya nchi hiyo imekuwa mbaya kiasi kwamba, serikali imeshindwa kuwalipa mishahara wafanyakazi wake na wanajeshi kwa miezi kadhaa sasa, suala ambalo limeibua malalamiko makubwa ya kijamii katika nchi hiyo yaliyoambatana na migomo na rangaito. Hivi karibuni nchi hiyo ilikaribia kutumbikia katika mgogoro mkubwa baada ya kundi la wanajeshi kuanzisha uasi wakitaka kulipwa malimbikizo ya mishahara na marupurupu yao. Hata hivyo mgogoro huo ulifikia tamati baada ya serikali kuahidi kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

Filihali, katika mazingira ambayo Ufaransa inahesabiwa kuwa mshirika wa kwanza wa kiuchumi wa Ivory Coast, hapana shaka kuwa, kuimarisha na kupanuliwa uhusiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili hizo hususan kuongezwa uwezekezaji vitega uchumi wa nchi hiyo ya bara Ulaya katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, ni jambo ambalo linaweza kumpa nguvu Rais Alassane Ouattara ya kuboresha hali ya nchi hiyo na hivyo kuwafanya raia wazidi kumuunga mkono. Ufaransa kwa upande wake si tu kwamba, itatumia fursa hiyo kwa ajili ya kuboresha uchumi wake kwa kustafidi na vyanzo vya utajiri na nguvukazi ya bei rahisi ya nchi hiyo, bali pia itayatumia mazingira hayo kwa ajili ya kuwapiku washindani wake na hivyo kuwa na uwepo mtawalia katika eneo la magharibi mwa Afrika na kujiandalia mazingira ya kunufaika na anga ya kisiasa na kiuchumi.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Suala la usalama na vita dhidi ya ugaidi ni ajenda nyingine iliyokuwa katika mazungumzo ya Marais wa Ivory Coast na Ufaransa. Kuenea harakati za makundi ya kigaidi katika ukanda wa Afrika Magharibi kwa upande mmoja na kuongezeka vitisho na operesheni za kigaidi nchini Ufaransa na katika nchi nyingine za Ulaya kwa upande mwingine, ni mambo ambayo yameifanya serikali ya Paris ilizingatie katika siasa za kigeni suala la kupambana na ugaidi. Ufaransa ambayo yenyewe kimsingi imekuwa muungaji mkono mkuu wa makundi ya kigaidi na kuwa mstari wa mbele katika kuzusha na kukuza hitilafu za kikaumu, kikabila na kidini katika nchi mbalimbali kama Iraq na Syria, hivi sasa yenyewe imetumbukia katika shimo ililolichimba.

Kiujumla mazungumzo ya kwanza ya Marais Ouattar wa Ivory Coast na Emmanuel Macron wa Ufaransa yanaweza kuwa ashirio la azma ya Paris ya kuendelea kuweko katika koloni lake hilo la zamani katika nyanja mbalimbali. Hii ni katika hali ambayo, akthari ya wananchi wa Ivory Coast hawaridhishwi na utendaji wa Rais Ouattara katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kiusalama na wamekuwa wakikosoa himaya ya siri na dhahiri ya Ufaransa kwa Rais Alassane Ouattara.