Jun 17, 2017 14:25 UTC
  • Mapigano yazuka baina ya waandamani na polisi nchini Morocco

Maandamano makubwa ya wananchi wa Morocco huko kaskazini mwa nchi hiyo, leo yamegeuka kuwa uwanja wa mapigano kati yao na vikosi vya usalama vya nchi hiyo ya kaskazini magharibi mwa Afrika.

Taarifa zinasema kuwa, polisi wa mji wa al-Hoceima wa kaskazini mwa Morocco leo wamelazimika kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamaji wengi waliokuwa wakiandamana wakilalamikia kutiwa mbaroni Nasser Zefzafi, kiongozi wa maandamano ya kupinga ufisadi nchini humo.

Maandamano ya wananchi hao yaliyoanza tangu siku ya Alkhamisi katika mji wa al-Hoceima yangali yanaendelea na yamepelekea kukwama shughuli nyingi za kawaida katika mji huo. Maandamano hayo yanatajwa kuwa makubwa zaidi kuwahi kutokea nchini Morocco tangu mwaka 2011.

Maandamano ya wananchi wa Morocco katika mji wa al-Hoceima

Hatua ya polisi ya mji wa al-Hoceima ya kuingilia maandamano hayo ya wananchi na kutumia mabomu ya gesi za kutoa machozi imezusha vurugu na mapigano kati ya waandamanaji hao na polisi. maduka mengi katika mji huo yamefungwa kwa siku kadhaa sasa.

Maandamano ya kupinga ufisadi yamekuwa yakifanyika nchini Morocco tokea mwaka jana wakati mchuuzi mmoja wa samaki aliposagwa na lori la kubeba taka wakati akijaribu kuchukua samaki wake waliokuwa wamechukuliwa na maafisa wa polisi kwa sababu alikuwa akiuza bidhaa sehemu isiyotakiwa.

Wanaharakati wanasema kuwa, maandamano ya hivi sasa ni muendelezo wa mwamko wa wananchi wa Morocco ulioanza sambamba na mwamko wa watu wa Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati mwaka 2011 na kupelekea madikteta kadhaa kungólewa madarakani.

Tags