UNICEF: Watoto 1,000 wanakimbia vita Sudan Kusini kila siku
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i30732-unicef_watoto_1_000_wanakimbia_vita_sudan_kusini_kila_siku
Huku ulimwengu leo ukiadhimisha Siku ya Wakimbizi duniani, imebainika kuwa watoto 1,000 kila siku hufurushwa makwao nchini Sudani Kusini.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Jun 20, 2017 13:43 UTC
  • UNICEF: Watoto 1,000 wanakimbia vita Sudan Kusini kila siku

Huku ulimwengu leo ukiadhimisha Siku ya Wakimbizi duniani, imebainika kuwa watoto 1,000 kila siku hufurushwa makwao nchini Sudani Kusini.

Hayo ni kwa mjibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF. Katika taarifa UNICEF imeongeza kuwa mgogoro wa Sudan Kusini sasa umegeuka na kuwa janga kwa watoto.

Aidha UNICEF imesema tangu kuanza kwa mgogoro huo mwaka 2013, zaidi ya watu milioni 1.8 wamevuka mpaka kutafuta hifadhi katika nchi jirani za Uganda, Ethiopia na Kenya, huku idadi kubwa zaidi ikiwa nchini Uganda. Shirika hilo kadhalika linasema hali katika nchi zinazohifadhi wakimbizi hao ni tete kwani zimezidiwa uwezo hasa Uganda ambayo inahifadhi zaidi ya wakimbizi nusu milioni.

Salva Kiir (kushoto) na Riek Machar

Takwimu hizi zinaripotiwa siku mbili kabla ya mkutano wa kimataifa wa mshikamano na wakimbizi mnamo Juni 22 hadi 23 nchini Uganda.  UNICEF imetahadahrisha kuwa asilimia 86 ya wakimbizi wote nchini humo ni wanawake na watoto na hivyo kuitolea wito jumuiya ya kimataifa kutoa fedha za usaidizi kwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambayo sasa inaongoza kwa idadi kubwa ya uhifadhi wa wakimbizi barani Afrika.

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba amehusika na jaribio la kuipindua serikali yake.