Waziri wa Sheria wa Misri alazimishwa kujiuzulu kufuatia matamshi yake ya kufuru
Hatimaye Waziri wa Sheria wa Misri, Ahmed al-Zand ambaye siku chache zilizopita pia aliibua matamshi ya utata, amelazimika kujiuzulu mara hii ikiwa ni baada ya kutoa matamshi ya kufuru na ya kumvunjia heshima Mtume wa Uislamu (saw). Al-Zand amejiuzulu baada ya Waziri Mkuu wa Misri Sherif Ismail kumtaka afanye hivyo.
Ijumaa iliyopita waziri huyo wa sheria alitoa matamshi ya utata kupitia kanali moja ya televisheni, ambayo yaliibua makelele ndani na nje ya nchi hiyo. Ahmed al-Zand alichaguliwa katika nafasi hiyo mwaka jana akimrithi mwanasiasa na jaji Mahfouz Saber aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo. Hata hivyo jaji Mahfouz Saber alienguliwa katika nafasi hiyo na Waziri Mkuu wa Misri baada ya kutoa matamshi yaliyoibua hasira kwa raia wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika pale aliposema kuwa, watoto wa masikini hawafai kuwa majaji wa nchi hiyo. Hivi sasa al-Zand anang'atuka uongozini katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja kutokana na matamshi yake machafu sawa na ya mtangulizi wake. Hata hivyo sababu ya kupigwa kalamu nyekundu al-Zand haiwezi kulinganishwa na ile ya Mahfouz Saber, hasa kwa kuzingatia kuwa Ahmed al-Zand alimvunjia heshima Mtukufu Mtume Muhammad (saw). Suala la kuzingatiwa hapa kuhusu mwanasiasa huyo ni kwamba, akiwa kama Waziri wa Sheria alifanya kosa hilo dhidi ya Mtume wa Uislamu, ndani ya nchi ambayo asilimia 91 ya raia wake ni Waislamu, huku Mtume Muhammad (saw) akiwa ni mmoja wa shakhsia wanaoheshimiwa na kuenziwa zaidi baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni wa nchi hiyo. Ama nukta nyingine ni hii kwamba, mbali na kutoa matamshi ya kufuru, kabla ya hapo pia Ahmed al-Zand aliwahi kutoa matamshi ya kichochezi na kupelekea kuibuka kwa wimbi la malalamiko ya wananchi na wanaharakati wa kisiasa dhidi yake, hata hivyo hakujiuzulu katika nafasi hiyo. Mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016, alitoa matamshi ya viishito kuwa kamwe hangetulia hadi pale atakapohakikisha wanachama elfu 10 wa Ikhwanul Muslimin wanauawa mkabala na kuuawa kwa askari jeshi na polisi mmoja wa nchi hiyo. Aidha al-Zand alisema mara tu baada ya kutolewa hukumu ya adhabu ya kifo dhidi ya aliyekuwa rais wa Misri, Muhammad Mursi, kuwa angesimamia utekelezwaji wa hukumu hiyo haraka iwezekanavyo. Kwa hakika matamshi hayo ya kijuba yanaashiria ni namna gani shakhsia huyo alivyo na fikra za kibaguzi na chuki ya hali ya juu dhidi ya Uislamu, jambo ambalo bila shaka linamvua ustahiki wa kuwa Waziri wa Sheria nchini Misri ambako raia wake wengi ni Waislamu. Suala muhimu kumuhusu al-Zand ni kwamba, baada ya kuteuliwa kuhudumia nafasi ya Waziri wa Sheria nchini Misri, raia wa nchi hiyo walionyesha upinzani wao mkali juu ya uteuzi huo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba raia hao waliamini kuwa si tu kwamba mwanasiasa huyo amezama katika dimbwi la ubaguzi, bali hakuwa na tofauti kubwa na mtangulizi wake Mahfouz Saber.