Jul 01, 2017 13:16 UTC
  • Wanachama saba wa ash-Shabab watiwa kitanzi nchini Somalia

Viongozi wa kijeshi katika eneo la Puntland, kaskazini mwa Somalia, wamewanyonga wanachama saba wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab.

Aul Ahmed Farah, mkuu wa mahakama ya kijeshi katika eneo hilo amesema kuwa, wanachama hao saba wa kundi hilo lenye mahusiano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaidah, wamenyongwa kwa kupatikana na hatia za kula njama za kutaka kuiondoa madarakani serikali ya Mogadishu. 

Wanachama wa kundi la kigaidi la ash-Shabab Somalia

Farah ameongeza kuwa, watu watano kati ya hao saba walitiwa mbaroni wakati wakisafirisha mada za miripuko kwenda katika eneo la Bosaso, katikati mwa mji wa Puntland, huku watu wengine wawili wakihusika na mauaji dhidi ya wakazi wa mji wa Galkayo, katikati mwa Somalia.

Hivi karibuni watu wenye mahusiano na kundi la ash-Shabab walivamia kambi ya kijeshi eneo lililo umbali karibu kilometa 100 kusini mwa mji wa Bosaso, ambapo katika hujuma hiyo watu 59 waliuawa. Kundi la kigaidi na ukufurishaji la ash-Shabab limekuwa likipigana tangu mwaka 2007 kwa lengo la kutaka kuiondoa madarakani serikali ya Somalia.

Hujuma za kundi hilo ndani ya Somalia

Mwaka 2011 kundi hilo lilipoteza udhibiti wa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu kufuatia kuzidiwa na askari wa Umoja wa Afrika (AMISOM) kwa kushirikiana na askari wa serikali ya nchi hiyo. Licha ya hayo kundi hilo bado limeendelea kutishia usalama wa mji huo kwa kuratibu mashambulizi ya mara kwa mara. 

Tags