Wafanyakazi wa UNICEF watekwa nyara Sudan Kusini
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, wafanyakazi watatu wa shirika hilo wametekwa nyara nchini Sudan Kusini.
Taarifa ya UNICEF imesema, watu waliotekwa nyara walikuwa wafanyakazi wa shirika la Montrose Corporation linaloshirikiana na Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kutoa elimu na mafunzo kwa watoto wadogo. Imeongeza kuwa, watu hao walitekwa nyara baada ya mapigano makali yaliyotokea tarehe 6 mwezi huu wa Julai nchini Sudan Kusini.
Awali UNICEF ilikuwa imetangaza kuwa, karibu watoto elfu 16 wanahudumu katika jeshi nchini Sudan Kusini na kwamba 800 miongoni mwao walisajiliwa mwaka uliopita wa 2016.
Sudan Kusini ilijitenga na Sudan mwaka 2011, na miaka miwili baadaye ikatumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.