Ndege za kivita za Marekani zauwa raia 18 Syria
Ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Marekani kwa mara nyingine tena zimeua raia 18 katika mji wa Raqqah kaskazini mwa Syria.
Raia 18 wa Syria wakiwemo watu nane wa familia moja jana waliuawa katika mji wa Raqqah katika mashambulizi ya ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Marekani.
Duru za habari za wapinzani wa Syria zimeripoti kuwa, raia wa Syria 189 waliuliwa mwezi Julai mwaka huu pekee katika mji wa Raqqah katika mashambulizi ya ndege za kivita za muungano unaoongozwa na Marekani nchini humo.
Ndege hizo mara kwa mara zimekuwa zikiwaua raia wa Syria wasio na hatia wala ulinzi kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi. Habari nyingine zinasema kuwa raia watatu wa Syria akiwemo mtoto mmoja, wameuawa na wengine 13 kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na magaidi katika maeneo yaliyo chini ya mzingiro katika mji wa Deir -Zor mashariki mwa Syria.
Maeneo ya makazi ya raia katika mji huo yamekuwa yakikabiliwa na mashambulizi ya mizinga ya makundi ya kigaidi kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Katika kujibu hujuma hizo, kikosi cha anga cha jeshi la Syria kimeshambulia maeneo wanapojikusanya magaidi wa kundi la Daesh huko magharibi mwa mji wa Deir-Zor na kuwaangamiza magaidi wengi na kuwasababishia hasara na maafa magaidi hao.