Mapigano makali yaikumba Sudan Kusini karibu na mpaka na Ethiopia
(last modified Fri, 11 Aug 2017 16:14:31 GMT )
Aug 11, 2017 16:14 UTC
  • Mapigano makali yaikumba Sudan Kusini karibu na mpaka na Ethiopia

Mapigano makali yameripotiwa kujiri leo katika mji wa Pagak nchini Sudan Kusini karibu na mpaka wa nchi hiyo na Ethiopia wakati waasi walipoanzisha mashambulizi dhidi ya askari jeshi wa serikali.

Msemaji wa waasi hao wa Sudan Kusini, Lam Paul Gabriel ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa wapiganaji kundi hilo wanapigana kuutwaa tena mji wa Pagak ambao ulitekwa na jeshi la serikali ya Juba tarehe 7 mwezi huu. Naye Dickson Gatluak Jock, msemaji wa vikosi serikali ya Sudan Kusini amethibitisha vikosi hivyo vishiriki katika mapigano hayo. Ameongeza kuwa, kikosi cha waasi wa  SPLA-IO kimekabiliwa na mashambulizi makali katika mji wa Pagak kutoka jeshi la serikali na kwamba lengo la waasi hao ni kuwafurusha wanajeshi hao kutoka katika mji huo wa kistratejia. 

Wanajeshi wa Sudan Kusini wakielekea katika mji wa kistratejia wa Pagak  

Siku sita zilizopita Jeshi la serikali ya Sudan Kusini lilifanikiwa kutwaa ngome kuu ya waasi katika eneo la Pagak lililoko karibu na mpaka wa nchi hiyo na Ethiopia. Mapigano ya kutekwa eneo hilo yamewalazimisha maelfu ya wakazi wa mji huo kukimbia nyumba na makazi yao. Eneo hilo limekuwa likidhibitiwa na waasi wa Sudan Kusini tangu mwaka 2014.

Eneo la Pagak ambalo liko katikati ya makazi ya watu wa kabila la Nuer, limekuwa kituo kikuu cha operesheni za waasi wa Sudan Kusini tangu mwaka 2014.