Mar 18, 2016 16:39 UTC
  • Morocco yaendelea kulalamika dhidi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco Salahuddin Mizwar, amesema nchi yake ina hitilafu na malalamiko dhidi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa binafsi.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco amesema, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon anapaswa kuwaheshimu watu wa Morocco. Mizwar ameongeza kuwa Sahara ya Magharibi kwa Morocco ni suala la kufa na kupona.

Kauli hiyo imekuja baada ya safari ya wiki iliyopita ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika kambi ya wakimbizi wa Sahara Magharibi karibu na eneo la Tindouf nchini Algeria ambapo aliwaeleza wakimbizi hao kwamba anaelewa fika hasira na uchungu walionao wananchi wa Sahara Magharibi kutokana na ardhi yao kuendelea kukaliwa kwa mabavu na Morocco.

Wakati huohuo serikali ya Rabat jana iliwataka wafanyakazi 84 wa kimataifa wa ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Sahara Magharibi waondoke katika eneo hilo ndani ya muda wa siku tatu kufuatia mzozo uliozuka kati ya serikali hiyo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Kufuatia hitilafu hizo juu ya suala la Sahara Magharibi, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amefuta safari yake nchini Morocco.

Siku ya Jumapili iliyopita mamia ya Wamorocco waliandamana kulalamikia matamshi ya Ban Ki-moon kwamba Sahara Magharibi ni eneo linalokaliwa kwa mabavu.

Serikali ya Rabat imemtuhumu Ban Ki-moon kuwa ameshindwa kuheshimu nafasi yake ya kutakiwa kutopendelea upande wowote katika mgogoro wa Sahara Magharibi na kwamba katika historia ya Umoja wa Mataifa hakuna Katibu Mkuu aliyewahi kutoa matamshi kama hayo ambayo kwa mujibu wa serikali ya Morocco yanakinzana na maazimio ya Baraza la Usalama la umoja huo.../

Tags