Aug 28, 2017 07:17 UTC
  • Mgogoro wa kisiasa nchini Sudan Kusini na kuendelea mapigano

Mgogoro wa kisiasa na mapigano katika nchi ya Sudan Kusini yanaendelea katika hali ambayo, kwa akali watu 40 wameuawa na kujeruhiwa katika mapigano mapya yaliyotokea kati ya jeshi la nchi hiyo na waasi katika jimbo la Yei.

Hii ni katika hali ambayo, Umoja wa Mataifa umesisitiza katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba, vita haribifu vya ndani huko Sudan Kusini, hadi sasa vimepelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa na kujeruhiwa. Aidha taarifa hiyo ya Umoja wa Mataifa imezitaka pande kuu hasimu katika mgogoro wa Sudan Kusini kufanya hima na juhudi katika mkondo wa kurejesha amani na maridhiano.

Sudan Kusini ilitumbukia katika machafuko na mapigano kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir na makamu wake wa zamani Riek Machar tangu mwaka 2013. Salva Kiir alimtuhumu makamu wake huyo kwamba, alipanga njama za kufanya mapinduzi. Baada ya kushadidi mgogoro huo na kwa juhudi za kieneo na kimataifa mwaka 2015 pande mbili zilifikia makubaliano ya kugawana madaraka. Hata hivyo kukiukwa vipengee vya makubaliano hayo, kulipelekea kuvunjika makubaliano hayo na kwa mara nyingine nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ikatumbukia katika vita na machafuko.

Wananchi wa Sudan Kusini wamekuwa wakitaabika kutokana na ukosefu wa huduma muhimu kama maji 

Filihali, ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa zinaonyesha juu ya kuweko mauaji ya kimbari katika nchi hiyo. Mgogoro na machafuko nchini Sudan Kusini yanaripotiwa kushadidi katika hali ambayo, hali ya kibinadamu katika nchi hizo inazidi kuwa mbaya. Kwa sasa nchi hiyo inakabiliwa na matatizo mengi ambapo bei ya vyakula iko juu, uchumi umezorota, kuna uhaba wa madaktari na dawa hali ambayo imeufanya mgogoro wa nchi hiyo kuchukua mkondo mpana zaidi. 

Jean-Pierre Lacroix, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya kusimamia amani amesisitiza katika ripoti yake kuhusiana na Sudan Kusini kwamba: Hali ya uchumi Sudan Kusini inasikitisha na kuendelea ukosefu wa amani na vitendo vya umwagaji damu katika nchi hiyo kumeifanya hali ya mambo iwe ya hatari na yenye kutetereka zaidi kwa wananchi na wakazi wake.

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini

Weledi wa mambo wanasema kuwa, mgogoro wa Sudan Kusini unapaswa kuchunguzwa kupitia sababu za ndani na za nje.  Katika upande wa ndani, kuweko muundo wa kikabila na kikaumu, kutokuwa na maandalizi ya kiutamaduni na kijamii, kutokuweko na ustawi na maendeleo ya kisiasa na kutokuweko miundombinu ya lazima ni mambo ambayo yameifanya nchi hiyo isiweze kupitia mkondo sahihi baada ya kujitangazia uhuru na mamlaka ya kujitawala mwaka 2011.

Rais Salva Kiir anatoka katika kabila la Dinka ambalo ndilo kabila kubwa zaidi nchini humo, huku hasimu wake na makamu wake wa zamani Riek Machar akiwa anatoka kabila dogo la Nuer. Kwa kuzingatia kwamba, katika nchi za Kiafrika ni ada na mazoea kwa mtu kufungamana na kabila lake, viongozi wa vyama na mahasimu wa kisiasa hutumbukia katika mapigano ya kikabila hususan panapokuweko msukumo wa kisiasa. Kwa kuzingatia ukweli huo, upande mmoja wa vita hususan mauaji ya hivi sasa huko Sudan Kusini chimbuko lake ni mizozo na mivutano ya kikabila.

Riek Machar hasimu wa kisiasa wa Rais Salva Kiir

Hivi karibuni gazeti la Kifaransa la Le Monde liliandika katika moja ya matoleo yake kwamba: Wananchi wa Sudan Kusini wamegeuka na kuwa maadui baina yao.

Hata hivyo katika mzozo huu wa Sudan Kusini haipaswi kughafilika na nafasi ya uingiliaji wa kigeni. Madola makubwa ya Magharibi na Uzayuni sio tu kwamba, hayafanyi jitihada za kuboresha hali ya mambo katika nchi hiyo, bali yanafanya njama ili mgogoro huo upanuke na kuenea katika maeneo mengine. Kugawanywa nchi na kisha kuenezwa mgogoro katika maeneo yaliyogawanywa ni mpango ambao unafuatiliwa na baadhi ya madola ya Magharibi na washirika wake barani Afrika.

Sudan Kusini nayo haijasalimika na mtego huu na inaonekana kwamba, hivi sasa imegeuzwa na kufanywa kuwa wenzo wa kisiasa wa kudhamini maslahi haramu ya madola ya Magharibi na waitifaki wake katika eneo la Afrika Mashariki. Katika mazingira kama haya raia wa Sudan Kusini ndio wahanga wakuu wa vita vya kuwania madaraka.

Tags