FAO yatoa wito wa kuweko uwekezaji wa kudumu nchini Uganda
(last modified Thu, 31 Aug 2017 14:21:17 GMT )
Aug 31, 2017 14:21 UTC
  • FAO yatoa wito wa kuweko uwekezaji wa kudumu nchini Uganda

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetoa wito wa kuweko uwekezaji wa kudumu katika nchi ya Uganda iliyoko katika eneo la Afrika Mashariki.

José Graziano da Silva, Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) amesema kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kusaidia mchakato wa uwekezaji wa kudumu nchini Uganda hususan katika sekta ya kilimo.

Ameongeza kuwa, Uganda inapaswa kusaidiwa hasa katika sekta ya kilimo, nchi ambayo imekuwa ikipokea kwa wingi wakimbizi kutoka nchi jirani hasa kutoka Sudan Kusini.

José Graziano da Silva, Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambaye hivi karibuni alizitembelea kambi za wakimbizi kaskazini mwa Uganda ameisifu na kuipongeza serikali ya Rais Yoweri Museveni kutokana na kuwapokea kwa moyo mkunjufu wakimbizi wanaoelekea katika nchi hiyo.

Wakimbizi wa Sudan Kusini waliokimbilia chini Uganda

Imeelezwa kuwa, Uganda inahitajia msaada wa kiasi cha dola bilioni mbili kwa mwaka ili iweze kukidhi mahitaji muhimu ya wakimbizi walioko katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, idadi ya raia wa Sudan Kusini waliokimbilia katika nchi jirani ya Uganda imefikia milioni moja.

Huku kukiweko na ripoti kwamba, Uganda imeanza kulemewa na mzigo wa wakimbizi hao kutoka Sudan Kusini, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linazitaka nchi wahisani kutoa misaada zaidi ya kibinadamu kwa ajili ya wakimbizi hao.

 

Tags