UN: Ethiopia inakabiliwa na Janga la njaa linaloweza kuongezeka
(last modified Wed, 06 Sep 2017 03:42:09 GMT )
Sep 06, 2017 03:42 UTC
  • UN: Ethiopia inakabiliwa na Janga la njaa linaloweza kuongezeka

Uwekezaji wa kina unahitajika ili wakazi wanaokabiliwa na njaa kutokana na ukame uliokithiri katika jimbo la Somali nchini Ethiopia waweze kustahimili ukame wa mara kwa mara unaosababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo imetolewa mjini Addis Ababa, Ethiopia na viongozi wa mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Chakula na Kilimo, FAO, Maendeleo ya Kilimo, IFAD na Mpango wa Chakula Duniani, WFP baada ya ziara yao ya siku nne nchini humo ambapo wamejionea mikakati ya kuepusha vifo vya mifugo sambamba na mgao wa chakula kwa watu wanaokabiliwa na njaa.

José Graziano da Silva, wa FAO, Gilbert F. Houngbo, wa IFAD na David Beasley wa WFP wametaka uwekezaji kwenye miradi ambayo itawezesha jamii kuhimili ukame wakisema kuwa ukame haupaswi kushughulikiwa kidharura kwa kuwa umekuwepo kwa muda mrefu sasa.

Baadhi ya miradi ambayo mashirika hayo yanatekeleza kwa kushirikiana na serikali ili kukwamua wananchi ni pamoja na ile ya umwagiliaji, vitalu vya matunda na vituo vya afya kwenye eneo la Tigray ambayo kwa pamoja imeongeza kipato, lishe na ufanisi  kwenye ukanda huo.

Ukame wa muda mrefu nchini Ethiopia umesababisha watu wapatao milioni 8.5 kuhitaji msaada wa chakula, huku maisha ya wafugaji yakituama kutokana na mifugo yao kufa hasa kwenye jimbo la Somali zamani, likijulikana kama Ogaden.