Mapigano yashuhudiwa kaskazini mwa Misri, Daesh watangaza kuhusika
Mapigano makali yalishuhudiwa hapo jana kati ya watu wenye silaha na askari wa serikali nchini Misri katika eneo la karibu na mji wa El Arish, kaskazini mwa nchi hiyo.
Mapigano hayo yalitokea baada ya watu wenye silaha kulishambulia gari la wanajeshi waliokuwa wanaenda kuwasaidia askari wenzao katika eneo la El-Safa, katika mji huo wa El-Arish. Katika hujuma hiyo askari wanne waliuawa na wengine tisa kujeruhiwa. Aidha ripoti zinaarifu kuwa, mapigano makali kati ya askari na watu wenye silaha yameshuhudiwa katika eneo la El-Safa, mapigano ambayo yamesababisha mauaji ya watu kadhaa. Kundi la kigaidi la Daesh tawi la Sinai, limetangaza kuhusika na shambulio hilo. Aidha watu 50 wameripotiwa kujeruhiwa katika eneo la al-Masurah katika kivuko cha Rafah, kaskazini mwa rasi ya Sinai nchini Misri. Hadi sasa usalama ni tete katika eneo la El-Safa, kufuatia askari kuimarisha doria kwa ajili ya kuwasaka washukiwa wa kundi hilo la kitakfiri. Itakumbukwa kuwa, eneo la Sinai liligeuka kuwa uwanja wa hujuma za watu wenye silaha, baada tu ya kuondolewa madarakani rais wa zamani za Misri muhammad Mursi anayeendelea kuzuiliwa katika jela na makamanda wa jeshi la nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.