Sep 09, 2017 16:27 UTC
  • Mapigano mapya yaibuka kati ya wanamgambo wa Seleka nchini CAR

Duru za usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati zimeripoti habari ya kujiri mapigano mapya kati ya waasi wa zamani wa kundi la Seleka katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapigano hayo yamejiri katika mji wa Bria, mashariki mwa Jamhuri ya Afrika ya Kati kati ya matawi mawili hasimu ya kundi hilo la Seleka na kusababisha makumi ya wapiganaji wa pande mbili kuuawa na kujeruhiwa. Shirika lisilo la kiserikali la madaktari wasio na mpaka linaloendesha shughuli zake katika maeneo ya mashariki mwa nchi sambamba na kutoa taarifa hiyo limetangaza kuwa, uingiliaji wa askari wa kofia ya buluu wa Umoja wa Mataifa, haukusaidia kuzuia kushtadi mapigano hayo mjini Bria.

Wapiganaji wa Seleka nchini CAR

Mapigano kati ya makundi hasimu ya wabeba silaha katika miezi ya hivi karibuni yamesababisha maelfu ya raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati kuwa wakimbizi. Mapigano na machafuko nchini humo vinatajwa kuongezeka katika hali ambayo kuna askari elfu 10 wa kusimamia amani wa Umoja wa Mataifa ambao wameshindwa kudhibiti hali ya mambo. Mapigano ya Jamhuri ya Afrika ya Kati yalianza mwaka 2013 baada ya waasi wa Seleka kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo François Bozizé.

Tags