Askari wa Kongo washambuliana na wakimbizi wa Burundi, makumi ya wakimbizi wauawa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34439-askari_wa_kongo_washambuliana_na_wakimbizi_wa_burundi_makumi_ya_wakimbizi_wauawa
Mapigano yamejiri kati ya wakimbizi wa Burundi na askari wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mashariki mwa nchi hiyo na kusababisha maafa ya makumi ya wakimbizi na wengine kujeruhiwa.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Sep 16, 2017 09:26 UTC
  • Askari wa Kongo washambuliana na wakimbizi wa Burundi, makumi ya wakimbizi wauawa

Mapigano yamejiri kati ya wakimbizi wa Burundi na askari wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mashariki mwa nchi hiyo na kusababisha maafa ya makumi ya wakimbizi na wengine kujeruhiwa.

Josué Boji, mmoja wa viongozi wa mkoa wa Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa, jumla ya wakimbizi 34 wa Burundi wameuawa na wengine 124 kujeruhiwa. Habari zaidi zinasema kuwa mapigano hayo yamejiri katika eneo linaloitwa Kamanyola, katika mkoa wa Kivu Kusini. Josué Boji ameongeza kuwa, Ijumaa ya jana askari wa nchi hiyo walikusudia kutawanya kundi la wakimbizi lililokuwa linaandamana kwa kufyatua risasi hewani, hata hivyo wakimbizi hao walianza kuwashambulia askari kwa kuwapiga mawe.

Polisi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Kwa mujibu wa Boji, kundi hilo la wakimbizi lilikusanyika kutaka kuachiliwa huru wenzao wanne waliokuwa wametiwa mbaroni tangu Jumatano usiku. Wakimbizi wa Burundi waliingia nchini humo baada ya kushtadi mzozo wa kisiasa nchini mwao mwaka 2015. Maeneo ya mashariki na kaskazini mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamekuwa yakishuhudia machafuko kwa kipindi cha miaka 20 sasa. Udhaifu wa jeshi la serikali na askari wa kofia ya buluu wa Umoja wa Mataifa, unatajwa kuwa chanzo cha ongezeko la machafuko maeneo hayo.