Sep 20, 2017 14:00 UTC
  • Watu 25 wauawa na kujeruhiwa katika mapigano Sabratha, Libya

Kituo cha operesheni dhidi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) kimeelezea habari ya kuendelea mapigano makali kati ya askari wanaosimamiwa na Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo na askari wanaoitwa 'Wanamapambano dhidi ya Daesh' chini ya komandi ya Khalifa Haftar, kamanda wa jeshi la kitaifa la nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa na kituo hicho imesema kuwa, katika mapigano hayo ya pande mbili karibu watu 10 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa. Kabla ya hapo ilitangazwa habari ya kuwepo mpango wa usitishaji mapigano kwa upatanishi wa viongozi wa kikabila wa eneo la Zintan. Hata hivyo juhudi hizo ziliambulia patupu ambapo muda punde tu baada ya usitishaji mapigano, kuliibuka makabiliano makali kati ya pande mbili hizo.

Mapigano makali nchini Libya

Jumapili iliyopita mji wa Sabratha, magharibi mwa Libya ulishuhudia mapigano makali ya pande mbili hizo na kupelekea watu kadhaa kuuawa na kujeruhiwa. Libya imekuwa uwanja wa machafuko tangu Jumuiya ya Kijeshi ya Nchi za Magharibi NATO kwa kuongozwa na Marekani, kuingilia kijeshi nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika na kumuondoa madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Tangu wakati huo, nchi hiyo imekosa usalama huku makundi ya kigaidi hususan Daesh (ISIS) yakitumia machafuko hayo kujipenyeza ndani ya taifa hilo.

Tags