Watu saba wauawa katika mlipuko wa bomu Mogadishu, Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i34983-watu_saba_wauawa_katika_mlipuko_wa_bomu_mogadishu_somalia
Watu wasiopungua saba wanaripotiwa kufariki dunia katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko mkubwa katika eneo moja mjini humo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 29, 2017 04:11 UTC
  • Watu saba wauawa katika mlipuko wa bomu Mogadishu, Somalia

Watu wasiopungua saba wanaripotiwa kufariki dunia katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya kutokea mlipuko mkubwa katika eneo moja mjini humo.

Polisi ya Somalia imetangaza kuwa, mlipuko huo wa bomu la kutegwa garini ulitokea jana katika Wilaya ya Hamarweyne na kwamba, hadi sasa haijajulikana mtu aliyetega bomu hilo. Hata hivyo vyombo vya usalama vya Somalia vinaamini kuwa, huenda bomu hilo likawa limetegwa na wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabab.

Meja Nur Hussein, afisa wa polisi mjini Mogadishu amewaambia waandishi wa habari kwamba, hadi sasa idadi ya watu waliouawa katika mlipuko huo ni saba na kwamba, majeruhi wanaendelea kupata matibabu.

Meja Nur Hussein amesema kuwa, mlipuko huo ulitokea wakati basi la abiria lilipokuwa likipita katika eneo hilo na kwamba, kuna uwezekano idadi ya wahanga wa shambulio hilo la kigaidi ikaongezeka.

Wanamgambo wa al-Shabab wa Somalia

Kundi la kigaidi la al-Shabab lilianzisha mashambulizi yake nchini Somalia mwaka 2006 ambapo kutokana na mashambulizi ya jeshi la serikali ya nchi hiyo kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika AMlSOM, lililazimika kukimbia kutoka mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu na kuelekea maeneo mengine ya mbali.

Licha ya operesheni ya pamoja ya jeshi la Somalia na kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini humo AMISOM kuonekana kupata mafanikio, lakini kundi hilo la kitakfiri lingali linadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.