Iran na Afrika Kusini zaafikiana kuendelea kuimarisha uhusiano
Afrika Kusini na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimeafikiana kuhusu kuimarisha uhusiano wa nchi mbili katika sekta mbali mbali.
Hayo yamebainika katika taarifa ya mwisho ya Kikao cha 13 cha Tume ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya Iran na Afrika Kusini. Kikao hicho kimefanyika leo katika mji wa Pretoria nchini Afrika Kusini na kuhudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Maite Nkoana-Mashabane na mwenzake wa Iran Mohamad Javad Zarif. Katika kikao cha tume hiyo pande mbili zimejadili na kutiliana saini hati za ushirikiano katika sekta za kilimo, uvuvi, uchukuzi,usafiri wa baharini na angani, uhusiano wa kibenki, uwekezaji na nano teknolojia.
Akizungumza na waandishi habari baada ya utiaji saini huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini amesema uhusiano wa nchi yake na Iran ni mzuri. Aidha aimesema Afrika Kusini inaunga mkono mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji na kuongeza kuwa Iran imefungamana na mapatano hayo na hilo limethibitishwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Tehran inaunga mkono ustawishaji uhusiano na Afrika Kusini katika sekta za kisiasa na kiuchumi. Aidha amesema Afrika Kusini ina umuhimu wa kipekee kwa Iran. Zarif pia ametoa radiamali yake kwa matamshi ya Rex Tillerson Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ambaye amesema: "Wale waliohusika katika vita dhidi ya ISIS nchini Iraq sasa warejee makwao." Zarif amesema wale waliopambana dhidi ya ISIS wako katika nyumba zao na wala hawatasubiri amri ya Marekani kwani iwapo wangekuwa wanasuburi amri ya serikali ya Marekani hivi sasa magaidi wa ISIS wangekuwa wanashikilia miji ya Baghdad na Erbil.