UN yaanza kuwahamisha wakimbizi wa Kiafrika kutoka Libya hadi Niger
Umoja wa Mataifa umeanza zoezi la kuwahamisha wakimbizi wa nchi za Afrika walioko Libya na kuwapeleka nchini Niger.
William Spindler, msemaji wa Shirika la Kuwahudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR ameliambia shirika la la habari la AFP kuwa, makumi ya wakimbizi hao ambao walikuwa katika hali mbaya ya kibinadamu wamegurishwa kutoka Libya hadi Niger, ili kunusuru maisha yao.
Amesema miongoni mwa wakimbizi hao ni wanawake 15, watoto wadogo wanne na wanaume sita, aghalabu yao wakiwa ni raia kutoka nchi za Eritrean, Ethiopian na Sudan.
Vincent Cochetel, Mjumbe Maalumu wa UNHCR katika maeneo yanayopakana na bahari ya Mediterranean amesema wakimbizi hao wamepekekwa katika vyumba vya wageni katika mji wa Niamey, na watasalia huko hadi mchakato wa kuwarejesha katika nchi zao ukamilike.
Zoezi hilo limeanza masaa machache baada ya wahajiri 73 kufa maji katika bahari ya Mediterranean wakati walipokuwa wanajaribu kuelekea Italia kutokea Libya.
Kwa mujibu wa takwimu za UN, raia wa Kiafrika wapatao 152,000 wamehatarisha maisha yao katika safari hatari za kuelekea barani Ulaya kutafua ajira na maisha kupitia bahari ya Mediterranean, ambapo zaidi ya elfu tatu miongoni mwao wamepoteza maisha ima kwa kuzama baharini, au kufa kwa njaa na kiu jangwani wakisubiri kusafirishwa.