Miili ya watu 11 waliofariki dunia katika ajali ya ndege Tanzania yapatikana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i36441-miili_ya_watu_11_waliofariki_dunia_katika_ajali_ya_ndege_tanzania_yapatikana
Miili ya abiria 10 na rubani mmoja waliopoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea jana nchini Tanzania imepatikana.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 16, 2017 16:05 UTC
  • Miili ya watu 11 waliofariki dunia katika ajali ya ndege Tanzania yapatikana

Miili ya abiria 10 na rubani mmoja waliopoteza maisha katika ajali ya ndege iliyotokea jana nchini Tanzania imepatikana.

Vyombo vya habari vimemnukuu Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo akisema shughuli ya kutafuta miili hiyo imekwenda vizuri na sasa maiti hizo zimepelekwa mkoani Arusha kwa ajili ya kuhifadhiwa.

Amesema: "Tuliwaomba wenyeji kulala hapa usiku kucha ili kuilinda miili hiyo isiliwe na wanyama na leo tumeikuta miili hiyo salama."

Watu hao walikuwa wakisafiri ndani ya ndege aina ya Cessna Grand Caravan ya kampuni ya Coastal Air, wakitoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kwenda kwenye uwanja wa ndege wa Sorenera uliopo kwenye Hifadhi ya Serengeti mkoani Mara.

Moja ya ndege za shirika la Coast air

Duru za habari zinasema kuwa, baadhi ya abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo walikuwa watalii waliofika nchini Tanzania kuona vivutio mbalimbali, kabla ya ajali hiyo kutokeo katika eneo la Bonde la Empakaai lililopo kwenye Hifadhi ya Ngorongoro mkoani Arusha.  

Mkurugenzi wa kampuni ya Coastal Air, Julian Edmunds, amesema kuwa wameshtushwa na ajali hiyo na kuongeza kuwa: “Tumekuwa tukirusha ndege yetu mara kwa mara, tuna imani na marubani wetu lakini pia tuna imani na ndege yetu.

Ajali hii inakuja ikiwa ni wiki tatu tangu ilipotokea ajali nyingine ya ndege ya Coastal ambapo watalii wawili walijeruhiwa huku wengine tisa waliokuwa kwenye ndege hiyo wakitoka salama.