Wasiwasi wa UN kuhusu hali ya wakimbizi wa Congo DR
Ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema kuwa, watu karibu milioni 2 wamelazimika kuhama makazi yao mwaka huu pekee huko katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kuhofia ukatili na mauaji.
Ripoti iliyotolewa na Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, kwa mwaka wa pili mfululizo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa na idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani duniani baada ya nchi za Syria na Yemen.
Wakimbizi wa ndani huko Congo wanakabiliwa na hali mbaya na maafa makubwa kwa kadiri kwamba, wengi miongoni mwao wanasumbuliwa na matatizo yanayotokana na kukosa huduma za tiba, chakula na maji ya kunywa. Msemaji wa Idara ya Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa, Yvon Edoumou ametahadharisha kuhusu hali mbaya inayowakabili wakimbizi wa ndani nchini humo na kusema: Misaada michache ya fedha zinazotolewa na wafadhili na jumuiya za masuala ya kibinadamu haiwezi kukidhi mahitaji ya wakimbizi hao. Edoumou ameongeza kuwa maafisa wa serikali ya Congo pia hawako tayari kushirikiana na pande husika kwa ajili ya kuondoa matatizo ya wakimbizi hao na wamebana shughuli za kufikisha misaada ya kibinadamu kwa watu wanaohitajia.
Maafa ya kibinadamu yanayokaribia kutokea katika maeneo yenye idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ongezeko la wimbi la wakimbizi katika nchi jirani, mgogoro mkubwa wa wakimbizi katika eneo la Maziwa Makuu na maeneo mengine ya dunia na hatari ya harakati za makundi ya waasi ni miongoni mwa mambo yanayozidisha wasiwasi wa jumuiya na taasisi za kimataifa kuhusu wakimbizi wa Congo.
Kwa miaka kadhaa sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inasumbuliwa na migogoro ya kisiasa na kiusalama kufuatia ghasa na machafuko ya ndani. Mkwamo wa kisiasa uliotokana na kuahirishwa mara kadhaa zoezi la uchaguzi wa rais na kushadidi harakati za makundi ya waasi hususan katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ni miongoni mwa mambo yanayozidisha machafuko na kuwalazimisha raia kukimbia makazi na nyumba zao.
Tahadhari ya Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa wakimbizi wa ndani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imetolewa huku nchi hiyo ikiendelea kusumbuliwa na migogoro chungu nzima ya kisiasa. Wakati huo huo askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wameshindwa kudhibiti hali ya mambo na kurejesha amani katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo. Hali hii imewafanya baadhi ya wachambuzi wa siasa wahusishe kufeli uko na siasa za madola makubwa ambayo yanapendelea kuvua samaki katika maji machafu na kwa msingi huo hayataki kuona amani inarejea katika maeneo ya mashariki mwa Congo yenye utajiri mkubwa wa madini hususan almasi. Madola hayo ya Magharibi yamekuwa yakipora utajiri wa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia maajenti na washirika wao.
Inaonekana kuwa iwapo mgogoro wa kisiasa wa Congo hautatatuliwa kwa kuitishwa uchaguzi huru na katika wakati mwafaka, nchi hiyo itaendelea kushuhudia matatizo ya wakimbizi na maafa ya kibinadamu.