Tunisia: Tumejiweka imara kukabiliana na ugaidi wa kitakfiri
Serikali ya Tunisia imetangaza kuchukua hatua maalumu kwa ajili ya kukabiliana na wimbi la magaidi wa kitakfiri nchini humo.
Wizara ya Masuala ya Dini nchini Tunisia imetangaza kuwa, mpango huo utaendele kutekelezwa kwa uchache kwa muda wa mwaka mmoja ambapo pia utajumuisha uangalizi wa mitandao ya kijamii na vyombo vya habari na pia shule na baadhi ya misikiti ambayo imekuwa ikitumiwa na magaidi katika kueneza mafundisho yao ndani ya taifa hilo. Weledi wa masuala ya dini nchini humo wanaamini kwamba, badala ya kutatua masuala ya kiusalama, serikali inatakiwa kwanza kutatua matatizo ya kijamii kupitia mafundisho ya utamaduni na kukabiliana na makundi yenye kufurutu ada. Inaelezwa kuwa, kushindwa kuwateua maimamu wa jamaa wenye kustahili katika kutoa mafundisho sahihi ya dini ya Kiislamu, kumekuwa na taathira hasi katika juhudi ya kukabiliana na makundi yenye kufurutu mipaka ya Mawahabi, suala ambalo limechangia vijana wengi kujiunga na magenge ya kigaidi. Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Tunisia, hadi sasa maelfu ya raia wa nchi hiyo, wamejiunga na makundi ya kigaidi katika nchi za Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika.