Dec 14, 2017 15:53 UTC
  • HRW: Polisi wa Kenya waliwabaka wanawake wakati wa uchaguzi

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema makumi ya wanawake walibakwa na maafisa wa polisi wakati wa msimu wa uchaguzi mkuu mwaka huu nchini Kenya.

Mtafiti mkuu wa masuala ya wanawake wa shirika hilo, Agnes Odhiambo amesema aghalabu ya kesi hizo za kubakwa wanawake na maafisa usalama waliovalia sare zao, huku wakiwa wamejizatiti kwa silaha zilifanyika katika mitaa ya mabanda ya Mathare, Dandora, na Kibera katika mji mkuu Nairobi, na kaunti zinazooenekana kuwa ngome za upinzani za Kisumu na Bungoma, magharibi mwa nchi.

Naye Tina Alai, wakili wa shirika hilo lenye makao yake makuu mjini New York amesema ni jambo la kusikitisha kuona maafisa usalama wanaopaswa kuwadhaminia usalama raia ndio wanaohusika na jinai dhidi ya raia wenyewe.

Maafisa wa polisi Kenya wakikabiliana na waandamanaji

Mmoja wa wahanga wa jinai hizo ni mwanamke wa miaka 28 aliyekuwa mjamzito kutoka mtaa wa Mathare, viungani mwa jiji la Nairobi, ambaye amesimulia kisa cha kusikitisha akisema: "Maafisa wanne wa polisi walivunja mlango na kuingia nyumbani kwangu kwa nguvu. Wanangu walikuwa wamelala, walimvuta mume wangu chini na kisha mmoja wao akanibaka huku wengine wakiwa wananikandamiza na kunipiga bakora. Nilivuja damu sana na mimba yangu ya miezi minne ikaharibika."

Oktoba mwaka huu, mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch na Amnesty International yalisema polisi ya Kenya imeua watu wasiopungua 67 katika maandamano ya upinzani ya kushinikiza mabadiliko kwenye Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, kuelekea uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 uliosusiwa na mrengo mkuu wa upinzani NASA.

 

Tags