UNICEF: Watoto Sudan Kusini wanakabiliwa na hali mbaya
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetahadharisha kuhusu hali mbaya ya watoto katika nchi ya Sudan Kusini.
Ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi wa UNICEF katika Masuala ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Leila Pakkala imesema kuwa, zaidi ya nusu ya watoto wa Sudan Kusini wameathiriwa na hali ya ukosefu wa amani.
Pakkala ameongeza kuwa, utapiamlo, maradhi, kusajiliwa kwa nguvu jeshini, ukatili na kunyimwa fursa ya kupata elimu ni miongoni mwa mashaka makuu ya watoto wa Sudan Kusini.
Afisa huyo wa UNICEF ametahadharisha kuhusu vitisho vilivyopo dhidi ya kizazi kijacho cha Sudan Kusini na ametoa wito wa kuchukuliwa hatua haraka za kulinda watoto nchini humo.
Sudan Kusini iliyojitenga na Sudan mwaka 2011 ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013 baada Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu aliyekuwa makamu wake, Riek Machar kwamba alifanya jaribio la kupindua serikali yake.