Rais wa Tunisia afanya mkutano wa kusitisha maandamano
Rais wa Tunisia amevunja kimya chake na kufanya mkutano na vyama vya siasa, miungano ya wafanyakazi na shirikisho la waajiri kwa shabaha yan kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa kiuchumi na maandamano yanayoshuhudiwa nchini humo kwa siku kadhaa sasa.
Katika ufunguzi wa mkutano huo wa jana Jumamosi, Rais Beji Caid Essebsi wa Tunisia amevituhumu vyombo vya habari vya Magharibi kuwa vinalichafulia jina taifa hilo kwa 'kutia chumvi' katika habari zinazohusiana na maandamano hayo.
Baada ya kikao hicho cha takriban masaa mawili, Mkuu wa Shirikisho la Waajiri UTICA, Wided Bouchamaoui amewaambia waandishi wa habari kwamba, hamna kitu cha maana kilichofikiwa baada ya mazungumzo ya jana, lakini wanatazamia kuwa serikali itatekeleza mapendekezo waliyoyatoa.
Malalamiko ya wananchi wa Tunisia yalianza mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari na kushtadi wiki iliyopita, baada ya serikali ya Tunis kupasisha sheria ya kuongeza bei za bidhaa na kukata ruzuku.
Serikali ya Tunisia imekumbwa na nakisi kubwa ya bajeti kutokana na kuporomoka thamani ya sarafu ya nchi hiyo, hivyo imeamua kutekeleza siasa za kubana matumizi, jambo ambalo limesababisha kushuhudiwa mfumko wa bei za bidhaa muhimu.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, karibu watu 800 wametiwa nguvuni nchini Tunisia tangu Jumatatu iliyopita hadi hivi sasa, mbali na mtu mmoja kuuawa katika machafuko hayo ya hivi karibuni.