Ethiopia yamuachia huru kinara wa upinzani, wafungwa 115
Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Ethiopia ambaye alikuwa gerezani ameachiwa huru, ikiwa ni jitihada za serikali za kutekeleza ahadi yake ya kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa.
Merara Gudina, kiongozi wa chama cha upinzani cha Oromo Federalist Congress alikamatwa mwaka jana aliporejea kutoka Ulaya, wakati nchi hiyo ilikuwa chini ya sheria ya hali ya hatari.
Gudima ameachiwa huru pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa wapatao 115, ambapo wamepokelewa kwa shangwe na maelfu ya wafuasi wao katika eneo la Burayu, viungani mwa mji mkuu Addis Ababa.

Idadi kamili ya wafungwa wa kisaisa wanaoshikiliwa katika jela za Ethiopia haijulikani lakini aghlabu yao walikamatwa katika ghasia na maandamano dhidi ya serikali ya nchi hiyo katika maeneo ya Amhara na Oromo tangu mwezi Agosti mwaka 2015 wakilalamikia kubaguliwa.
Watetezi wa haki za binadamu wanasema kuwa karibu wafungwa elfu mbili wa kisiasa wangali wanashikiliwa katika jela za Ethiopia.
Siku chache zilizopita Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn alitangaza mpango wa serikali wa kufuta mashitaka dhidi ya wafungwa wote wa kisiasa sambamba na kufunga jela ya kuogofya ambako wafungwa hao walikuwa wanazuiliwa.