UNICEF yatahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya watoto Sudan Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39253-unicef_yatahadharisha_kuhusiana_na_hali_mbaya_ya_watoto_sudan_kusini
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetahadharisha kuhusu hali mbaya inayowakabili watoto katika nchi changa ya Sudan Kusini.
(last modified 2025-11-19T08:00:07+00:00 )
Jan 21, 2018 03:11 UTC
  • UNICEF yatahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya watoto Sudan Kusini

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetahadharisha kuhusu hali mbaya inayowakabili watoto katika nchi changa ya Sudan Kusini.

Sambamba na indhari hiyo, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesisitiza kwamba, mustakabali wa wananchi wa Sudan Kusini upo hatarini.

Shirika hilo limeashiria asilimia 70 ya watoto wa Sudan Kusini waliokosa fursa ya kwenda shule na kubainisha kwamba, kizazi kipya cha nchi hiyo changa zaidi barani Afrika  kinakabiliwa na hatari ya kukosa fursa ya kusoma.

Aidha taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imebainisha kwamba, watoto katika maeneo ya kaskazini mwa Sudan Kusini wanakabiliwa na hali mbaya ya lishe duni na kwamba, kizazi kipya cha nchi hiyo kitaangamia endapo hakutachukuliwa hatua za kukiunga mkono na kukisaidia.

Raia wa Sudan Kusini wakikimbia makazi yao

Sudan Kusini ilitumbukia katika vita vya ndani mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kuipindua serikali yake.

Kufuatia vita na mapigano hayo, maelfu ya raia wa nchi hiyo wamelazimika kuwa wakimbizi huku mamia ya wengine wakiuawa na kujeruhiwa.

Ripoti mbalimbali za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba, hali ya kibinadamu nchini humo ni mbaya na kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua za kweli za kuwasaidia raia wa nchi hiyo wanaohitajia mno misaada ya chakula.