Jan 26, 2018 07:18 UTC
  • Shambulizi la 'ISIS' laua makumi ya watu nchini Mali

Makumi ya watu wameripotiwa kupoteza maisha katika shambulizi la bomu la kutegwa ardhini linaloaminika kufanywa na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) nchini Mali.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo kwa jina Abdoulaye Cheick amenukuliwa na waandishi wa habari akisema kuwa, watu 24 wakiwemo watoto wadogo wanne wamethibitishwa kuaga dunia katika shambulio hilo la jana Alkhamisi, katika mji wa Boni, katikati ya Mali.

Kanali Diarran Kone, msemaji wa Jeshi la Mali amesema gari la abiria lililokanyaga bomu hilo la kutegwa ardhini lilikuwa likitokea katika nchi jirani ya Burkina Faso na lilikuwa limebeba raia wa nchi mbili hizo za eneo la Sahel.

Awali maafisa wa serikali ya Mali walisema kuwa watu 13 pekee ndio wameuawa kwenye shambulizi hilo.

Ramani ya Mali

Nchi ya Mali inakumbwa na machafuko na mashambulizi ya kigaidi tangu mwaka 2012 wakati yalipotokea mapinduzi ya kijeshi na kuzuka uasi kaskazini mwa nchi hiyo, uliopelekea kutekwa  eneo kubwa la nchi hiyo na waasi.

Askari wa Umoja wa Mataifa pamoja na wale wa mkoloni Ufaransa walitumwa nchini Mali katikati ya mwaka 2013, lakini pamoja na hayo wameshindwa kuzima uasi huo na harakati za kigaidi licha ya kukomboa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yametekwa.

Tags