Ethiopia yawaachia huru wafungwa wengine zaidi ya elfu 2 wa kisiasa
Serikali ya Ethiopia imeendeleza wimbi la kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, mara hii ikiwaondoa gerezani maelfu ya wafungwa waliotuhumiwa kuhusika na machafuko yaliyolikumba eneo la Oromiya kati ya 2015 na 2016.
Rais wa eneo la Oromiya, Lema Megersa jana Ijumaa alisema wafungwa 2,345 wameachiwa, siku chache baada ya makumi ya wafungwa wengine kuachiwa huru, akiwemo kiongozi mkongwe wa upinzani katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Hivi karibuni, Merara Gudina, kiongozi wa chama cha upinzani cha Oromo Federalist Congress ambaye alikamatwa mwaka jana aliporejea kutoka Ulaya, wakati nchi hiyo ilikuwa chini ya sheria ya hali ya hatari, aliachiwa huru hivi karibuni pamoja na wafungwa wengine wa kisiasa wapatao 115.
Watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakisisitiza kuwa kuna zaidi ya wafungwa elfu mbili wa kisiasa ambao wangali wanashikiliwa katika jela za Ethiopia.

Siku chache zilizopita Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn alitangaza mpango wa serikali wa kufuta mashitaka dhidi ya wafungwa wote wa kisiasa sambamba na kufunga jela ya kuogofya ambako wafungwa hao walikuwa wanazuiliwa.
Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa uliitaka serikali ya Addis Ababa iangalie upya hali ya idadi kubwa ya wafungwa wa kisiasa wanaozuiliwa katika jela za nchi hiyo.