UN yaitaka serikali ya Kenya iheshimu uhuru wa vyombo vya habari
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i39845-un_yaitaka_serikali_ya_kenya_iheshimu_uhuru_wa_vyombo_vya_habari
Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Kenya kuheshimu agizo la mahakama lililoitaka ibatilishe hatua yake ya kuzifungia televisheni tatu kupeperushaji matangazo baada ya stesheni hizo kurusha moja kwa moja hafla ya kuapishwa kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo Raila Odinga.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 03, 2018 04:05 UTC
  • UN yaitaka serikali ya Kenya iheshimu uhuru wa vyombo vya habari

Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Kenya kuheshimu agizo la mahakama lililoitaka ibatilishe hatua yake ya kuzifungia televisheni tatu kupeperushaji matangazo baada ya stesheni hizo kurusha moja kwa moja hafla ya kuapishwa kiongozi wa upinzani wa nchi hiyo Raila Odinga.

Taarifa ya Shirika la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa sambamba na kulaani kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini Kenya, imeitaka pia serikali ya Nairobi kuheshimu uamuzi wa mahakama.

Wakati huo huo, Angela Quintal, Mshirikishi wa Mipango wa Afrika wa shirika la kutetea uhuru wa vyombo vya habari linalojiita 'Kamati ya Kuwalinda Wanahabari' yenye makao makuu yake mjini New York amesema Kenya inapaswa kuwa kitovu cha kulinda haki za wananchi kupata habari barani Afrika.

Kadhalika amemkosoa vikali Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, kwa kutolaani kitendo hicho cha serikali ya Kenya cha kuzima urushaji wa matangazo ya televisheni alipotoa taarifa ya kulaani hatua ya kuapishwa kwa Odinga hivi karibuni.

Stesheni za runinga zilizofungiwa na serikali

Urushaji matangazo wa vituo vitatu vya televisheni nchini Kenya umeendelea kusimamishwa licha ya amri ya Mahakama Kuu ya nchi hiyo kuiamuru serikali iondoe zuio hilo.

Jaji Chacha Mwita wa mahakama hiyo aliitaka Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo kurejesha upeperushaji wa matangazo ya moja kwa moja ya televisheni hizo, hadi kesi kuhusu kadhia hiyo itakaposikilizwa na kuamuliwa Februari 14.