Feb 06, 2018 03:16 UTC
  • Watu 30 wauawa katika mapigano ya kikabila Kongo DR

Watu zaidi ya 30 wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyotokea katika mkoa wa Ituri huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mapigano hayo mapya kati ya makabila ya Hema na Lendu yaliripuka Ijumaa iliyopita mkoani Ituri, mashariki mwa nchi hiyo.

Hadji Ibrahim Ruhigwa Bamaraki, msemaji wa kabila la Hema sambamba na kulaani mapigano hayo ya kikabila, ameyataja mauaji hayo kama ya ugaidi.

Mauaji yanaendelea ushuhudiwa Kongo DR licha ya uwepo wa askari wa kimataifa

Amesema mbali na watu 12 kujeruhiwa vibaya, vijiji kadhaa vya mkoa huo vimeteketezwa kwa moto na kusababisha familia kati ya 500 na 800 kuachwa bila makazi.

Duru za habari jana Jumatatu ziliripoti kuwa, watu zaidi ya 23 wa kabila la Hema na 10 wa kabila la Lendu wameuawa katika kijiji cha Djugu mkoani Ituri, kutokana na mapigano kati ya makabila hayo mawili hasimu.

Wafugaji wa kabila la Hema na wakulima kutoka kabila la Lendu wamekuwa wakizozana kwa miongo kadhaa sasa, ambapo maelfu ya watu wa makabila hao waliuawa kati ya mwaka 1999 na 2003.

 

 

Tags