Feb 08, 2018 03:59 UTC
  • Magaidi wanne watiwa mbaroni katikati ya Somalia

Jeshi la Somalia limetangaza habari ya kutiwa mbaroni magaidi wanne wa genge la wakufurishaji la al Shabab, katikati ya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Jeshi hilo limeongeza kuwa, magaidi hao wanne waliowekwa nguvuni jana (Jumatano) wanashukiwa kuhusika katika mauaji ya kamishna wa zamani wa eneo la Bulo Burte katika eneo la Hiiraan, katikati ya Somalia. 

Kwa mujibu wa jeshi hilo, askari wa Somalia wamewatia mbaroni magaidi hao baada ya kugundua njama mpya za kuua viongozi wengine wa eneo la Hiiraan.

Wanajeshi wa Somalia wakiwa katika msako wa magaidi wa al Shabaab katika eneo la Hiiraan, katikati ya nchi hiyo

 

Kwa karibu miaka 30 sasa, Somalia imekuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na machafuko yasiyo na mwisho. Hivi sasa serikali kuu ya nchi hiyo inaungwa mkono na jamii ya kimataifa lakini imeshindwa kurejesha utulivu nchini humo. Hata Umoja wa Afrika umetuma askari wake nchini Somalia, lakini bado kunaendelea kuripotiwa mauaji, miripuko na vitendo vingine vya kigaidi.

Miongoni mwa miji inayoshambuliwa sana na magaidi wa al Shabab ni Beledweyne katika eneo la Hiiraan na hadi sasa askari wa Umoja wa Afrika chini ya mwavuli wa AMISOM na jeshi la Somalia wameshindwa kuwamaliza magaidi mjini humo.

Tags