UN: Wahajiri 22 wa Ethiopia watoweka baada ya kuzamishwa baharini
(last modified Sat, 10 Feb 2018 01:36:56 GMT )
Feb 10, 2018 01:36 UTC
  • UN: Wahajiri 22 wa Ethiopia watoweka baada ya kuzamishwa baharini

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limesema wahajiri 22 raia wa Ethiopia wanahofiwa kufa maji baada ya kutupwa baharini, katika pwani ya Yemen.

Joel Millman, msemaji wa IOM hapo jana alikiambia kikao cha Umoja wa Mataifa mjini Geneva kuwa, wahajiri hao walidondoshwa kwenye kina kikuu cha bahari katika pwani ya Yemen, na kulazimishwa kuogolea hadi ufuoni.

Amesema boti iliyokuwa imebeba Wahabeshi hao ni kati ya boti nne zilizowapeleka raia 602 wa Ethiopia katika eneo la Shabwa, pwani ya Yemen na kwamba wahajiri 22 hawajaweza kupatikana kufikia sasa.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, wahajiri 30 wa Kiafrika waliripotiwa kufariki dunia baada ya kuzama maji katika pwani ya Yemen, wakati wakielekea Djibouti.

Wahajiri wa Kiafrika katika safari za kutisha za baharini

Kwa mujibu wa IOM, zaidi ya watu 87,000 walihatarisha maisha yao katika safari hizo za baharini za kuogofya, wakijaribu kufika Yemen mwaka jana pekee.

Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) linasema zaidi ya wakimbizi elfu tatu waliaga dunia mwaka jana wakijaribu kufika Ulaya kupitia Bahari ya Mediterania, akthari ya wahajiri hao wakiwa ni raia wa nchi za Kiafrika ambao wanataraji kupata maisha mazuri na ajira katika nchi za barani Ulaya.