Shughuli za kijamii zalemazwa na mgomo Kongo Brazzaville
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4039-shughuli_za_kijamii_zalemazwa_na_mgomo_kongo_brazzaville
Harakati za kila siku za kijamii katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo, Brazzaville zimeathiriwa na mgomo uliotishwa na viongozi wa upinzani nchini humo, kulalamikia kuchaguliwa tena Rais Denis Sassou Nguesso.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 29, 2016 14:42 UTC
  • Shughuli za kijamii zalemazwa na mgomo Kongo Brazzaville

Harakati za kila siku za kijamii katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kongo, Brazzaville zimeathiriwa na mgomo uliotishwa na viongozi wa upinzani nchini humo, kulalamikia kuchaguliwa tena Rais Denis Sassou Nguesso.

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, maeneo mengi ya kijamii na ya burudani kama vile mahoteli na maduka yamesalia kufungwa mchana kutwa hii leo mjini hapo. Soko maarufu la Total ambalo ndilo kubwa zaidi mjini Brazzaville nalo halikufunguliwa hii leo. Mbali na Brazzaville, shughuli za kila siku zimeathiriwa pakubwa katika miji mingine ambayo ni ngome ya upinzani kama vile Bacongo, Makelekele na Kinsoundi. Hata hivyo maisha yameonekana kuendelea kama kawaida katika wilaya ya Poto-Poto ambayo inaaminika kuwa wakaazi wake wengi wanaunga mkono serikali ya Rais Nguesso. Jumapili iliyopita, viongozi watano wa upinzani nchini humo walioshindwa katika uchaguzi wa rais wa Machi 20 akiwemo Guy-Brice Parfit Kolelas aliyeibuka wa pili kwa kupata asilimia 15 ya kura na Jean-Marie Mokoko ambaye alishika nafasi ya tatu kwa asilimia 14 waliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maandamano ya amani ya nchi nzima hii leo, kupinga kuchaguliwa tena Rais Denis Sassou Nguesso mwenye umri miaka 72. Tume ya Uchaguzi nchini Kongo Brazzaville ilimtangaza Denis Sasso Nguesso kuwa mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi wa Machi 20 kwa kupata asilimia 60 ya kura zote halali zilizopigwa. Nguesso ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 30, Oktoba mwaka jana alibadilisha katiba na kuondoa kipengee kinachoweka ukomo wa vipindi viwili kwa Rais na kujiandalia mazingira ya kubakia madarakani.