Kujiuzulu Waziri Mkuu wa Ethiopia
Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa Ethiopia amejiuzulu kufuatia malalamiko na maandamano ya mara kwa mara ya watu wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika
Huku akibainisha kwamba amejiuzulu nafasi hiyo kwa hiari yake mwenyewe, Waziri Mkuu Desalegn amesema kuwa hali ya hivi sasa ya nchi hiyo inatia wasiwasi mkubwa na kusistiza kwamba matatizo ya nchi hiyo yanapaswa kutafutiwa ufumbuzi ambao hautaathiri usalama na uthabiti wake. Hailemariam Desalegn amejiuzulu katika hali ambayo ni kwa muda sasa ambapo nchi hiyo imekuwa ikishuhudia malalamiko na maandamano ya mara kwa mara ya wananchi dhidi ya serikali yake. Maandamano hayo yalianzia eneo la Oromia mwaka 2015 kutokana na hatua ya serikali ya kutwaa mashamba ya kilimo ya eneo hilo kwa kisingizio cha kupanua mji na kutekeleza miradi ya maendeleo, na kisha kuenea katika maeneo mengine ya nchi.

Oromo na Amhara ni makabila mawili makubwa ya Ethiopia ambayo yamekuwa yakilalamika kuwa yanabaguliwa na kutengwa na serikali. Yanalalamika kwamba serikali imekuwa ikiwatenga katika ugawaji wa nyadhifa muhimu serikalini na kulizingatia tu kabila la Tigray na hivyo kuyatenga kisiasa na kiuchumi makabila mawili hayo.
Hata kama malalamiko ya makabila hayo mawili makubwa ya Ethiopia yalikuwa yamezimwa kwa kiwango fulani kufuatia ukandamizaji wa askari usalama wa nchi hiyo na pia kutiwa nguvuni kwa vinara wa mrengo wa upinzani, lakini malalamiko hayo yaliibuka tena katika miji tofauti ya nchi hiyo miezi michache iliyopita. Ikiwa ni katika juhudi za kutuliza hali ya mambo, serikali ya Addis Ababa miezi kadhaa iliyopita ilichukua hatua ya kukarabati baraza la mawiri na kuwaachilia huru wafungwa kadhaa wa kisiasa lakini pamoja na hayo kuendelea ukandamiza wa polisi na askari usalama dhidi ya wapinzani na vilevile kutobadilishwa baadhi ya siasa kuu za serikali ni mambo yaliyosababisha kuendelea malalamiko na maandamano ya wapinzani.

Kwa kuzingatia hilo, wapinzani wanataka mabadiliko makubwa ya kisiasa na kijamii yafanyike na pia kukomeshwa ukiukaji wa haki za binadamu na hasa mauaji na kutiwa nguvuni kwa umati raia na vilevile kukomeshwa kutengwa kisiasa makundi ya wapinzani nchini. Ni kwa kuzingatia hali hiyo ya kutia wasiwasi ndipo Hailemariam Desalegn, Waziri Mkuu wa Ethiopia akaamua kujiuzulu huku akikiri udharura wa kufanyika mabadiliko hayo muhimu nchini. Wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa wanasema ni siasa zake mbovu ndizo zilizoifikisha Ethiopia katika hali hii ya kusikitisha na hivyo wamekaribisha kujiuzulu kwake. Kuhusiana na hilo, Abebe Gellaw, mwandishi wa Ethiopia anasema kuhusu sababu ya kujiuzulu Desalegn kwamba waziri mkuu huyo tayari alikuwa amepoteza udhibiti wa nchi muda mrefu uliopita, na hivyo kupelekea maeneo mengi ya nchi hiyo kutumbukia kwenye machafuko. Anasema Waethiopia wengi wamekuwa wakipiga makele ya kutaka kurejeshewa haki zao za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa sababu wanahisi kwamba wametengwa na serikali. Watu wengi wamepoteza maisha yao na maelfu ya wengine wanapitishia umri wao wakiwa kwenye jela za kuogofya za nchi hiyo.

Muhammad Adamou, mchambuzi mwingine wa masuala ya kisasa anasema kuwa kujiuzulu huko kwa Desalegn hakutokani na nia yake njema bali kunatokana na mashinikizo yasiyokoma ya wanamapambano wa kisiasa na kiuchumi wa nchi hiyo, ambayo yamekuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa sasa. Hata kama tunatarajia matukio muhimu ya kisiasa kutokea nchini Ethiopia katika siku zijazo lakini ni wazi kuwa wananchi wa nchi hiyo wanataka kuona mabadiliko hayo yakifanyika haraka iwezekanavyo, na bila shaka Waziri Mkuu wa nchi hiyo anapasa kuandaa uwanja wa kufanyika mabadiliko hayo ili kuiondoa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika katika mgogoro wa hivi sasa.