Kutangazwa hali ya hatari nchini Ethiopia
(last modified Sat, 17 Feb 2018 13:26:04 GMT )
Feb 17, 2018 13:26 UTC
  • Kutangazwa hali ya hatari nchini Ethiopia

Serikali ya Ethiopia imetangaza hali ya hatari nchini humo siku moja baada ya kujiuzulu Hailemariam Desalegn Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Viongozi wa Ethiopia wamesema kuwa hali ya hatari imetangazwa nchini humo kufuatia pendekezo la serikali kwa lengo la kulinda katiba na kuzuia kuzuka machafuko nchini humo. 

Katika miaka ya hivi karibuni Ethiopia imekumbwa na mivutano ya kisiasa na maandamano ya wananchi dhidi ya serikali. Ethiopia ilitumbukia katika mivutano ya kisiasa kutokana hatua zilizochukuliwa na serikali ya Addis Ababa na ubaguzi wa kikabila unaoonekana nchini humo. Makabila mawili ya Oromo na Amhara ambayo yanaunda zaidi ya asilimia 60 ya jamii ya watu wa Ethiopia yanalalamikia dhulma za kijamii na yanapinga siasa za serikali ya nchi hiyo mkabala na makabila hayo. Kutwaliwa ardhi za kilimo kulikofanyika kwa kisingizio cha kupanua mji mkuu kulichochea malalamiko ya wananchi mwaka 2015 huko Ethiopia na tangu wakati huo serikali ya Addis Ababa imekuwa ikikandamiza waandamanaji na kutangaza hali ya hatari nchini humo kwa shabaha ya kudhibiti hali ya mambo. 

Maandamano ya wananchi dhidi ya serikali yamepamba moto wakilalamika na kupinga siasa za kuchuja habari na taarifa, ukandamizaji, ukiukaji wa haki za binadamu, kutiwa mbaroni na utumiaji wa mabavu dhidi ya raia. Wapinzani wengi wa serikali ya Ethiopia wanaamini kuwa, serikali ya Addis Ababa  miezi kadhaa iliyopita na katika vipindi tofauti ilitekeleza sheria eti ya kupambana na ugaidi kwa lengo la kukandamiza wanaharakati wa kisiasa, waandishi habari na wafanya maandamano. Takwimu rasmi zilizotolewa na Kamisheni ya Haki za Binadamu nchini Ethiopia zinaonesha kuwa, zaidi ya raia 669 waliuawa katika maandamano ya wananchi ya mwaka juzi wa 2016. Wakati huo waandamanaji zaidi ya elfu 26 walitiwa nguvuni. 

Maandamano ya watu wa makabila ya Oromo na Amhara dhidi ya serikali 

Katika upande mwingine, matakwa ya wananchi na hali mbaya ya kisiasa nchini yamezusha hitilafu kati ya viongozi wa Ethiopia. Kujizulu ghafla kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Hailemariam Desalegn na kukiri kwamba kuna udharura wa kufanyika marekebisho nchini humo ni kielelezo kwamba, viongozi wa Ethiopia wenyewe wanahitilafiana kimitazamo kuhusu namna ya kutatua mgogoro unaoikabili nchi hiyo. 

Hailemariam  Desalegn, Waziri Mkuu aliyejiuzulu wa Ethiopia  
 

Abebe Gellaw mwandishi habari aliyeko uhamishoni nchini Eritrea ambaye ni raia wa Ethiopia amesema kuwa: Katika kipindi cha miaka 26 iliyopita kundi la waliowachache limekuwa likishikilia madaraka ya Ethiopia, na Hailemariam Desalegn alikuwa kibaraka wa kundi hilo. Sasa wananchi wanataka mabadiliko na Waziri Mkuu ajaye anapasa kufanya mabadliko hayo.  

Abebe Gellaw, mwandishi habari wa Ethiopia aliyeko uhamishoni nchini Eritrea 

Hii ni katika hali ambayo serikali ya Ethiopia haijachukua hatua yoyote ya kivitendo ya kushughulikia matakwa ya watu wake licha ya kupita muda sasa tangu kuanza maandamano dhidi ya serikali. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kutolewa tangazo la hali ya hatari ni silaha nyingine inayotumiwa na serikali ya Addis Ababa kwa ajili ya kubana zaidi anga ya kisiasa na kudhibiti hali ya mambo. 

Inaonekana kuwa hali ya amani na utulivu inaweza kurejeshwa nchini Ethiopia iwapo matakwa ya wananchi ya kufanyika  mageuzi ya kisiasa na kufutwa ubaguzi wa kikabila na kikaumu yatazingatiwa sambamba na kuandaliwa mazingira ya kiadilifu kwa raia wote wa nchi hiyo, kusitishwa ukandamizaji, kufunguliwa anga ya kisiasa na kuwepo uhuru wa vyombo vya habari.