Botswana yamtaka Kabila Ang'atuke madarakani Congo
Botswana imemtaka Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ang'atuke madarakani.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Botswana imesema kuwa hali mbaya inayoshuhudiwa hivi sasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inatokana na kiongozi wa nchi hiyo kuchelewesha uchaguzi na kushindwa kudhibiti nchi hiyo.
Taarifa hiyo imeihimiza jamii ya kimataifa kumuwekea mashinikizo zaidi kiongozi wa DRC ili ang'atuke madarakani na kutayarisha mazingira ya kujitokeza hali mpya ya kisiasa nchini humo.
Joseph Kabila alichukua madaraka ya nchi mwaka 2001 baada ya mauaji ya baba yake na alitarajiwa kuondoka madarakani 2016 baada ya kukamilisha vipindi viwili vya utawala kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mamia ya watu wameuawa kutokana na mapigano ya mara kwa mara kati ya jeshi la Congo DR na wapinzani wanaomtaka Rais Kabila ang'atuke madarakani.