Feb 27, 2018 14:07 UTC
  • Watu 22 wauawa Kongo katika mapigano ya kikabila

Kwa akali watu 22 wameuawa kwenye mapigano ya kikabila mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hope Sabini, afisa wa serikali mashariki mwa Kongo DR amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema kuwa, watu hao waliuawa baada ya kundi la waasi wa Nyatura ambao aghalabu yao wanatoka kabila la Wahutu kuvamia vijiji vya Kalusi na Bwalanda na kukabiliana na waasi wa genge la Mai Mai Mazembe siku ya Jumapili na jana Jumatatu.

Afisa huyo amebainisha kuwa, raia 11 wameuawa katika kijiji cha Kalusi, huku wengine wanne na waasi saba wakiuawa katika kijiji cha Bwalanda.

Eneo la Ituri mashariki mwa DRC limekuwa uwanja wa mapigano ya kikabila kwa miaka mingi

Hivi karibuni, Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (Unicef) ulisema kuwa, watu 76 wengi wakiwa ni wanawake na watoto wameuawa katika mapigano ya kikabila yaliyojiri katika mkoa wa Ituri nchini DRC kuanzia mwezi Disemba mwaka jana hadi sasa. 

Ni miaka ishirini imepita sasa ambapo maeneo ya mashariki na kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanashuhudia hali ya mchafukoge na ukosefu wa amani.

Tags