Mar 11, 2018 16:17 UTC
  • Mashambulizi mapya yasababisha kuuawa askari 2 na magaidi 16 Sinai, Misri

Wimbi jipya la mapigano katika Rasi ya Sinai nchini Misri limepelekea kuuawa wapiganaji 16 wa kundi la kigaidi na wanajeshi wawili wa serikali.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumapili, Msemaji wa Jeshi la Misri, Kanali Tamer Rifai amesema askari wawili wa serikali wameuawa huku wengine sita wakijeruhiwa katika operesheni ya hivi punde dhidi ya ngome za magaidi huko Sinai.

Ameongeza kuwa, ndege za kijeshi zimeshambulia ngome za magaidi hao katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Peninsula ya Sinai, pamoja na eneo la Nile Delta, na kufanikiwa kuangamiza wapiganaji 16.

Wanajeshi 18 wa Misri wameuawa tangu jeshi la nchi hiyo lianzishe operesheni ya kuwaangamiza waasi katika eneo la Sinai Februri 9 mwaka huu.

Magaidi katika Rasi ya Sinai, Misri

Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, vikosi vya ulinzi vya Misri vimefanikiwa kugundua maficho 1,907 ya magenge ya kigaidi na maghala yao ya silaha na mada za miripuko.

Operesheni kubwa ya jeshi na polisi wa Misri dhidi ya magenge ya kigaidi ilianza tarehe 9 Februari 2018 katika maeneo tofauti ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hususan katika Rasi ya Sinai.

Tags