Juhudi za kutaka kukomboa wasichana waliotekwa nyara nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41671-juhudi_za_kutaka_kukomboa_wasichana_waliotekwa_nyara_nchini_nigeria
Serikali ya Nigeria ina nia ya kuanza mazungumzo na kundi la kigaidi la Boko Haram katika jitihada za kutaka kuwakomboa wasichana 111 waliotekwa nyara hivi karibuni na kundi hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 14, 2018 23:56 UTC

Serikali ya Nigeria ina nia ya kuanza mazungumzo na kundi la kigaidi la Boko Haram katika jitihada za kutaka kuwakomboa wasichana 111 waliotekwa nyara hivi karibuni na kundi hilo.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Rais wa Nigeria imesema kuwa Muhammadu Buhari anataka wasichana hao waliotekwa nyara katika eneo la Dapchi huko kaskazini mashariki mwa Nigeria warejeshwe kwa familia zao wakiwa hai. Kwa msingi huo suala la kufanya mazungumzo na Boko Haram limewekwa katika ajenda ya serikali ya Abuja.

Tarehe 19 mwezi uliopita wa Februari wapiganaji wa kundi la Boko Haram walishambulia shule moja ya wasichana katika eneo la Dapchi kwenye jimbo la Yobe na kuteka nyara wasichama 111. Hii ni mara ya pili kundi hili linashambulia shule ya wasichana nchini Nigeria. Aprili mwaka 2014 wapiganaji wa kundi hilo la Boko Haram walishambulia shule ya wasichana ya Chibok na kuteka nyara wasichama 276 na hadi sasa hatima ya zaidi ya mia moja kati yao haijajulikana. 

Japokuwa katika miaka ya hivi karibuni jeshi la Nigeria limezidisha mapambano dhidi ya wapiganaji wa Boko Haram kwa shabaha ya kuliangamiza kabisa kundi hilo lakini hadi sasa wanachama wake wangali wanafanya mauaji ya hapa na pale, na wanawake, wasichana na watoto wadogo ndio waathirika wakubwa zaidi wa mashambulizi ya kundi hilo. Kundi hilo pia linawatumia watoto na wanawake wanaotekwa nyara katika mashambulizi ya kigaidi au kuolewa kwa kulazimishwa na kuwa watumwa wa ngono. 

Image Caption

Msemaji wa UNICEF, Marixie Mercado amesema: "Kundi la Boko Haram limezidisha mara nne kuwatumia watoto wadogo kama mabomu ya binadamu katika mashambulizi ya kigaidi huko kaskazini mwa Nigeria."

Japokuwa mashambulizi ya jeshi la Nigeria dhidi ya ngome za kundi la Boko Haram yamepelekea kuuawa idadi kubwa ya wanachama wa kundi hilo lakini kushadidi kwa mashambulizi ya wapiganaji wa kundi hilo pekee hakutoshi kwa ajili ya kuliangamiza kabisa genge hilo la kigaidi.

Itakumbukwa kuwa katika kampeni zake za uchaguzi wa rais, Rais Muhammadu Buhari aliahidi kuliangamiza kikamilifu kundi hilo kama angeshinda uchaguzi wa rais. Hata hivyo hivi sasa na baada ya kupita miaka kadhaa tangu achukue madaraka ya nchi, Buhari hajafanikiwa kutekeleza ahadi yake, na si hayo tu, bali kundi hilo limepanua zaidi mashambulizi yake hadi katika nchi jirani kama Cameroon, Niger na Chad. Wachambuzi wa mambo wanasema, udhaifu wa serikali kuu ya Nigeria, kutokuwepo irada na azma imara ya kupambana na ugaidi na ufisadi ndani ya taasisi za jeshi ni miongoni mwa sababu zinazozuia kuangamizwa kundi hilo la kigaidi. Sambana na hayo hatupasi kusahau nafasi ya nchi za Magharibi na washirika wao zinazowapa misaada ya siri magaidi hao na kuwatumia kwa shabaha ya kufikia malengo yao ya kikoloni.

Boko Haram

Alaa kulli hal, tunapaswa kusibiri na kuona juhudi za serikali ya Abuja za kutaka kuwakomboa wasichana 111 wanaoshirikiwa na Boko Haram zitafikia wapi.