Mar 24, 2018 15:59 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika mapigano mapya CAR

Duru za habari za Jamhuri ya Afrika ya Kati zimeripoti kuwa, kumezuka mapigano mapya kati ya makundi ya wabeba silaha na kupelekea watu kadhaa kuuawa, katika maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Katika mapigano hayo ambayo habari zinasema yalianza tangu siku tatu zilizopita, makundi ya wabeba silaha yamefanya mauaji ya wanawake kadhaa mbele ya umati wa watu na halafu kuzuia wasizikwe.

Katika miezi ya hivi karibuni, maeneo ya kaskazini magharibi mwa nchi hiyo ya katikati ya Afrika, yalishuhudia mapigano makali kati ya makundi ya wabeba silaha. Kabla ya hapo pia, nchi hiyo ilikumbwa na mapigano makali mno yaliyopelekea makumi ya maelefu kuuawa na mamia ya wengine kuwa wakimbizi. Wahanga wakuu wa mashambulizi hayo walikuwa ni Waislamu na maeneo yao hasa ya ibada.

Baadhi ya makundi ya wabeba silaha nchini CAR

Mapigano na machafuko nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati yanaendelea katika hali ambayo ndani ya nchi hiyo kuna maelfu ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wakiwemo pia maelfu ya askari wa nchi hiyo ambao wanaweza kuzuia mapigano na mauaji hayo. Hivi karibuni Rais Faustin-Archange Touadéra wa nchi hiyo aliutaka Umoja wa Mataifa kuongeza idadi ya askari wa kusimamia amani nchini mwake na kuwapatia silaha za kuwawezesha kudhibiti hali ya mambo nchini humo.

Tags