Mar 29, 2018 04:34 UTC
  • Waasi wauwa watu 11 kaskazini mashariki mwa Kongo

Waasi wenye silaha wamewauwa raia wasiopungua 11 katika shambulio moja kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Raia wengine wasiopungua elfu moja wameshauliwa na waasi hao hadi hivi sasa tangu mwaka 2014 katika mashambulizi kama hayo.

Meya wa mji wa Beni, Nyonyi Bwanakawa ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa raia hao waliuliwa juzi jioni na waasi wa ADF wa uganda katika mji wa Beni mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kituo cha Uenezaji Amani, Demokrasia na Haki za Binadamu katika mji wa Beni kimebainisha kuwa waasi wa ADF wamewauwa raia wasiopungua 11 kwa kutumia mapanga na nyundo.

Wasiwasi watanda karibu na mji wa Beni nchini Kongo kufuatia mashambulizi ya waasi wa ADF

Serikali na Umoja wa Mataifa umelaani mauaji mtawalia karibu na mji wa Beni tangu mwaka 2014; mengi yakifanywa na waasi wa ADF kwa silaha hatari huku wataalamu wa kujitegemea wakisema kuwa baadhi ya wanajeshi wa Kongo pia wanahusika katika mauaji hayo.

Mji wa Beni ni moja ya vitovu kadhaa huko mashariki na katikati mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambako wimbi la machafuko limezidisha wasiwasi na uwezekano wa nchi hiyo kutumbukia tena katika vita vya ndani.

Tags