Wapambe wa Mandela wamtaka rais Zuma ajiuzulu haraka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4294-wapambe_wa_mandela_wamtaka_rais_zuma_ajiuzulu_haraka
Mwanaharakati maarufu anayepinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini amemtaka Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo ang'oke madarakani haraka iwezekanavyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 02, 2016 12:02 UTC
  • Ahmed Kathrada (kulia) akiwa pamoja na hayati Nelson Mandela
    Ahmed Kathrada (kulia) akiwa pamoja na hayati Nelson Mandela

Mwanaharakati maarufu anayepinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini amemtaka Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo ang'oke madarakani haraka iwezekanavyo.

Ahmed Kathrada, ambaye pia alikuwa mtu wa karibu sana na hayati Nelson Mandela, rais wa zamani wa nchi hiyo amemtumia ujumbe Rais Jacob Zuma akimtaka ajiuzulu haraka. Amesema kuwa, ikiwa Zuma ataheshimu pendekezo hilo, basi ataisaidia serikali kuweza kujikwamua na mgogoro huo unaotokana na kukosa uaminifu kwake. Rais Jacob Zuma anakabiliwa na tuhuma za kuhusika na ufisadi wa kifedha, suala ambalo limezusha wimbi la ukosoaji mkubwa kutoka katika vyombo vya mahakama na uangalizi vya nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo wawakilishi wa chama cha Muungano wa Kidemokrasia katika bunge la Afrika Kusini, wamewasilisha pendekezo la kutokuwa na imani na uwezo wa kisiasa wa Rais Zuma katika bunge la nchi hiyo.

Tayari Rais Zuma kupitia televisheni, amewaomba radhi raia wa nchi hiyo kutokana na kupatikana na hatia za ufisadi wa fedha. Aidha ameahidi kurejesha katika hazina ya taifa kiwango cha fedha alichoamrishwa kurejesha serikali na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo.