Apr 18, 2018 04:05 UTC
  • HRW: Maafisa usalama na chama tawala wanaua wapinzani Burundi

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema maafisa usalama wakishirikiana na wafuasi wa chama tawala nchini Burundi CNDD-FDD wanawaua na kuwashambulia wapinzani hususan wanaoonekana kupinga kura ya maoni inayotazamiwa kufanyika mwezi ujao.

Taarifa ya jana Jumanne ya Human Rights Watch imesema kuwa, shirika hilo lenye makao yake mjini New York limethibitisha kutokea visa 19 vya kuhujumiwa wapinzani na wakosoaji wa serikali tangu Disemba 12 hadi sasa.

Hii ni katika hali ambayo, mapema mwezi huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilieleza wasiwasi wake kuhusiana na hali ya kisiasa nchini Burundi sambamba na ukosefu wa irada thabiti ya kisiasa ya kuupatia ufumbuzi mgogoro uliopo.

Taarifa ya rais wa baraza hilo ilizitaka pande husika za kisiasa nchini humo kushiriki pasina na masharti yoyote kwenye mazungumzo ya amani yanayoongozwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC.

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi

Mwezi uliopita, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi alitangaza Mei 17 kuwa tarehe ya kufanyika kura ya maoni ya kuifanyia mabadiliko katiba ya nchi.

Iwapo kwa uchache asilimia 50 ya wapiga kura wataunga mkono mabadiliko hayo ya katiba, watakuwa wamemsafishia njia Nkurunziza ambaye amekuwa madarakani tokea mwaka 2005, kusalia uongozini hadi mwaka 2034.

Tags