Polisi ya Rwanda yawakamata makumi ya wakimbizi wa Kongo DR
Polisi ya Rwanda imewatia nguvuni wakimbizi 23 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walioko nchini humo, kwa tuhuma za kuwashambulia kwa mawe maafisa waandamizi wa polisi na serikali, waliotembelea kambi yao.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, maafisa hao wa ngazi za juu wa usalama na serikali wa Rwanda walirushiwa mawe na wakimbizi katika kambi ya Kiziba siku ya Jumatatu, na kesho yake Jumanne, maafisa wa polisi walienda kambini hapo na kuanza kuwafyatulia mabomu ya kutoa machozi wakimbizi hao.
Desange Mukeshimana, mmoja wa wakimbizi hao wapatao 17,000 wa Kongo DR amenukuliwa na shirika hilo la habari akisema kuwa, maafisa wa polisi jana Jumanne waliingia kambini hapo kwa kishindo huku wakifyatua ovyo mabomu ya kutoa machozi na risasi hai na kupelekea mtoto mmoja kuuawa.
Hata hivyo polisi ya Rwanda kupitia msemaji wake, Theos Badege imekataa kuzungumzia suala hilo la iwapo walitumia risasi hai ua la dhidi ya wakimbizi hao, lakini inasisitiza kuwa wakimbizi kadhaa wamekamatwa kwa kuwashambulia maafisa usalama kwa mawe na vifaa venye ncha kali.
Itakumbukwa kuwa, Februari mwaka huu, polisi ya Rwanda iliua idadi kadhaa ya wakimbiizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo waliokuwa wakifanya maandamano mbele ya ofisi ya Umoja wa Mataifa, kupinga hatua ya UN ya kukata mgao wao wa misaada.
Polisi ya Rwanda hata hivyo ilisema ililazimika kutumia nguvu baada ya wakimbizi hao karibu elfu tatu kuanza kuwarushia mawe askari usalama.