Chama cha CUF: Hatumtambui Dakta Shein kama Rais wa Zanzibar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i4405-chama_cha_cuf_hatumtambui_dakta_shein_kama_rais_wa_zanzibar
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi CUF nchini Tanzania limetoa maazimio 13 baada ya kumaliza kikao chake cha siku mbili visiwani Zanzibar.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 04, 2016 12:01 UTC
  • Chama cha CUF: Hatumtambui Dakta Shein kama Rais wa Zanzibar

Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la Chama Cha Wananchi CUF nchini Tanzania limetoa maazimio 13 baada ya kumaliza kikao chake cha siku mbili visiwani Zanzibar.

Moja ya maazimio hayo ni kutoyatambua matokeo ya uchaguzi wa marudio wa Machi 20 lilioutaja kuwa ni haramu na batili, na kwa msingi huo hakimtambui Dk. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Zanzibar. Aidha CUF imesema, haitoshirikiana na Serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na Katiba ya Zanzibar, kinyume na Sheria ya Uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu. Azimio hilo limesema kwa vyovyote vile, Serikali itakayoundwa haitakidhi matakwa ya Katiba ya Zanzibar na hivyo CUF haitoshiriki kwenye uvunjaji wa Katiba ambayo inaeleza kwa uwazi kabisa namna ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

Azimio jingine la chama hicho linawataka wananchi wote wa Zanzibar kutumia njia za amani, za kikatiba na kisheria ambazo zimewahi kutumika katika nchi nyingine duniani kuwakataa watawala waovu na wasio na ridhaa ya watu waliojiweka madarakani kwa kutumia nguvu na ubakaji wa demokrasia kwa kutoipa ushirikiano Serikali itakayoundwa na watawala hao.

Azimio jingine la chama hicho linasema kuwa, baraza kuu la uongozi wa CUF linaendelea kuutambua uchaguzi mkuu uliokuwa halali, huru, wa haki na uliofanyika katika hali ya amani na utulivu wa tarehe 25 Oktoba, 2015 na pia linayatambua matokeo yake ambayo yalionesha wazi kwamba chaguo la Wazanzibari ni CUF na Maalim Seif Sharif Hamad kuiongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.