Maadamano ya wananchi Madagascar yailazimu mahakama kuu kufuta sheria mpya ya uchaguzi
Hatimaye Mahakama Kuu ya Katiba nchini Madagascar imefuta sehemu ya sheria mpya ya uchaguzi iliyoibua hivi karibuni ghasia na maandamano ya wananchi.
Mahakama hiyo Kuu ya Katiba mbali na kufuta baadhi ya sheria mpya za uchaguzi, imeyataja masuala yanayohusiana na kupitiwa daftari la wapigakura, muda wa kampeni za uchaguzi, mazingira ya lazima kwa ajili ya kujiandikisha wagombea katika uchaguzi wa rais na mambo mengine kuwa yanayokiuka katiba.

Tangu tarehe 21 Aprili, wapinzani wa Rais Hery Rajaonarimampianina wa Madagascar wamekuwa wakifanya maandamano wakitaka kubatilishwa sheria za uchaguzi zilizopasishwa hivi karibuni ambazo walizitaja kuwa na upendeleo. Kadhalika wapinzani walimtaka rais huyo kujiuzulu huku wakisema sio rais wa taifa hilo. Hayo yanajiri katika hali ambayo kumesalia miezi saba kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais na bunge, ambapo wapinzani wanaamini kwamba kupitishwa sheria zilizobatilishwa kulikuwa ni kwa maslahi ya Rais Hery Rajaonarimampianina na chama chake. Ravalomanana aliyewahi kuwa rais wa Madagascar anashirikiana na aliyemrithi kiti hicho, Andy Rajoelina, kupinga marekebisho na sheria za uchaguzi.