Raia karibu 700 wa Ethiopia waliokuwa wamefungwa Saudia warejeshwa kwao
(last modified Mon, 21 May 2018 07:52:41 GMT )
May 21, 2018 07:52 UTC
  • Raia karibu 700 wa Ethiopia waliokuwa wamefungwa Saudia warejeshwa kwao

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia imesema kuwa, karibu raia 700 wa nchi hiyo waliokuwa wamefungwa nchini Saudi Arabia, wamerejea nyumbani.

Wizara hiyo imetoa taarifa na kusema kuwa, raia 690 wa Ethiopia walikuwa wamefungwa jela huko Saudi Arabia wamerejeshwa nyumbani baada ya kufanyika mazungumzo baina ya Addis Ababa na Riyadh.

Wizara hiyo imeongeza kuwa, tayari raia hao 690 wameshapewa misaada ya fedha ya kuweza kuwafikisha katika maeneo na miji yao wanayoishi ndani ya Ethiopia.

 

Kila mwaka maelfu ya raia wa Ethiopia wanavuka Bahari Nyekundu na kuingia Saudi Arabia kwa ajili ya kutafuta kazi au kama njia ya kuelekea katika nchi nyingine.

Safari za Waithiopia hao zinakuwa za magendo, na mara nyingi wanakuwa hawana visa wala iqama ya kuishi ndani ya Saudi Arabia au katika nchi nyingine wanakokimbilia.